Tottenham wamnunua Fernando Llorente aliyekuwa anasakwa na Chelsea

Fernando Llorente Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Fernando Llorente alifunga mabao 15 Ligi ya Premia msimu uliopita

Tottenham wamekamilisha usajili wa mshambuliaji wa Swansea Fernando Llorente kwa mkataba wa miaka miwili kwa ada ambayo haijafichuliwa.

Mabingwa wa Ligi ya Premia Chelsea walikuwa wamekaribia kumchukua kwa £15m lakini mwishowe hawakufanikiwa.

Mchezaji huyo wa miaka 32 alicheza chini ya meneja wa sasa wa Chelsea Antonio Conte alipokuwa kwenye usukani klabu ya Juventus.

Lakini Mhispania huyo aliamua kwenda Spurs badala yake na kuwa mchezaji wa tano kusajiliwa na klabu hiyo katika dirisha la usajili lililofungwa usiku wa kuamkia leo.

Llorente alijiunga na Swansea Agosti 2016 na kufunga mabao 15 na kusaidia klabu hiyo kukwepa kushushwa daraja msimu uliopita.

Mchezaji huyo wa kimo cha futi 6 inchi 4 alikaa misimu tisa Athletic Bilbao, kabla ya kwenda Juventus na kukaa miaka miwili ambapo alishinda mataji mengi na kisha akakaa mwaka mmoja Sevilla.

Amefungia timu ya taifa ya Uhispania mabao saba katika mechi 24 na alishinda Kombe la Dunia mwaka 2010.

Ndiye wa tano kununuliwa na Spurs na alisajiliwa baada ya Serge Aurier kujiunga nao kutoka Paris St-Germain kwa £23m mapema Alhamisi.

Mshambuliaji Vincent Janssen atasalia kuwa mchezaji mwenzake Llorente baada ya Mholanzi huyo kukataa mpango wa kumpeleka Brighton kwa mkopo.

Mada zinazohusiana