Riyad Mahrez ashindwa kuondoka Leicester City

Riyad Mahrez Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Riyad Mahrez alijiunga na Leicester City kutoka klabu ya Le Havre mwaka 2014

Riyad Mahrez amesalia kuwa mchezaji wa klabu ya Leicester City baada ya kufungwa kwa dirisha la kuhama wachezaji bila yeye kufanikiwa kuhama.

Hii ilitokea hata baada yake kuachiliwa kutoka kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Algeria ili akashughulikie kuhama kwake kutoka Leicester.

Roma, ambao mwishowe waliacha kumtafuta tena Mahrez, walikuwa wamewasilisha dau mara tatu bila mafanikio baada ya mahrez kutangaza kwamba alitaka kuwahama mabingwa hao wa ligi msimu wa 2015-16.

Mchezaji huyo hata hivyo bado anaweza kuahmia Barcelona kwani dirisha la kuhama wachezaji litafungwa usiku wa Ijumaa.

Manchester United na Chelsea walimtaka pia mchezaji huyo wa miaka 26.

Shirikisho la soka la Algeria (FAF) lilisema Mahrez alikuwa amepewa ruhusa kuondoka kwenye kambi ya mazoezi Alhamisi ili kufanikisha mkataba kabla ya siku ya mwisho ya kuhama wachezaji.

Taarifa ya FAF ilisema Mahrez alipewa ruhusa na kocha wa timu ya taifa Lucas Alcaraz na FAF kwenda Ulaya kukamilisha uhamisho Alhamisi.

Timu ya taifa ya Algeria ilisafiri Alhamisi kwenda Lusaka kucheza dhidi ya timu ya taifa ya Zambia Jumamosi bila yeye.

Mahrez alitawazwa mchezaji bora chaguo la wachezaji baada ya kuchangia sana ufanisi wa Leicester msimu walioshinda ligi.

Amewachezea mechi zao zote Ligi ya Premia msimu huu.

Kiungo wa kati wa Leicester Nampalys Mendy, 25, amerejea timu yake ya awali ya Nice kwa mkopo wa msimu mmoja.

Danny Drinkwater naye amehamia Chelsea kuungana na N'Golo Kante.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii