Carlos Tevez aambiwa ni 'mnene' hawezi kucheza China

Carlos Tevez

Chanzo cha picha, Getty Images

Mshambuliaji wa Argentina Carlos Tevez ameambiwa na mkufunzi mpya wa klabu yake ya Shanghai Shenhua nchini China Wu Jingui kwamba ni mnene na hatachezea timu hiyo hadi apunguze uzani na kuwa sawa kucheza.

Tevez, 33, ambaye anaaminika kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa pesa nyingi zaidi duniani, amefunga mabao mawili pekee katika mechi 12 tangu alipoanza kuwachezea mwezi Machi.

Wu, aliyechukua usukani katika klabu hiyo baada ya Gus Poyet kujiuzulu Jumatatu, pia alimkosoa kiungo wa kati qFredy Guarin.

"Ninafaa kuwajibika kwa timu na kwa wachezaji," alisema Wu.

"Wote wawili (Tevez na Guarin) wana uzani uliozidi kiwango. unapokuwa uwanjani, ikiwa huwezi kucheza 100%, basi haina maana."

Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United na Manchester City alihamia Shanghai kutoka Boca Juniors.

Hata hivyo alikosa karibu nusu ya mechi za klabu hiyo msimu huu kutokana na majeraha.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Shanghai Shenhua wamo nafasi ya 12 Ligi Kuu ya China baada ya kucheza mechi 23 msimu huu

Alirejea China hivi majuzi baada ya ziara ya wiki mbili nchini Argentina ambako alikuwa ameenda kutibiwa tatizo la misuli.

"Nilizungumza naye leo kuhusu mbinu za kiufundi, lakini sitamruhusu kucheza kwa sasa, mwili wake hauko tayari," aliongeza Wu kwenye mahojiano na Shanghai Morning Post.