Kombe la Dunia Urusi 2018: Tiketi za kwanza zaanza kuuzwa

Russia 2018

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mechi ya kwanza itachezwa 14 Juni

Kundi la kwanza la tiketi za fainali za Kombe la Dunia 2018 ambazo zitachezewa nchini Urusi zilianza kuuzwa Alhamisi.

Mashabiki wa soka wanaweza kuwasilisha maombi ya kununua tiketi hizo kupitia tovuti ya Fifa.

Tiketi hizo zitauzwa kwa awamu mbili.

Bei ya tiketi hizo itakuwa ni kuanzia £79 kwa mechi za raundi ya pili hatua ya makundi hadi £829 kwa fainali yenyewe ambayo itachezewa Moscow.

Kwa kufuata sera za awali za uuzaji wa tiketi, wakazi wa urusi watakuwa na aina maalum za tiketi ambazo bei yake itaanzia £17.

Tiketi ghali zaidi zitakuwa za mechi ya fainali yenyewe ambazo zitauzwa £829.

Hilo litakuwa ni ongezeko la £151 ukilinganisha na tiketi za mechi sawa za fainali ya mwaka 2014 ambayo ilichezewa Rio de Janeiro nchini Brazil.

"Tumeweka mfumo wa kutoa tiketi ambao utawapa mashabiki nafasi sawa ya kujipatia tiketi," katibu mkuu wa Fifa Fatma Samoura amesema.

*bei imehesabiwa kutoka kwa Dola za Marekani hadi kwa Pauni za Uingereza kwa kutumia viwango vya sasa vya ubadilishanaji wa fedha.

**bei imehesabiwa kutoka kwa Ruble za Urusi hadi kwa Pauni za Uingereza kwa kutumia viwango vya sasa vya ubadilishanaji wa fedha.

Awamu ya kwanza ya kuwasilisha maombi ya tiketi itafanyika kabla ya tarehe 12 Oktoba.

Watakaowasilisha maombi watafahamishwa kufikia 16 Novemba iwapo wamefanikiwa.

Michuano hiyo itaanza tarehe 14 Juni ambapo Urusi wakicheza mechi ya ufunguzi uwanjani Luzhniki, Moscow.

Mataifa saba yamejikatia tiketi ya kushiriki michuano hiyo pamoja na mwenyeji Urusi - mabingwa mara tano Brazil, Ubelgiji, Iran, Mexico, Japan, Saudi Arabia na Korea Kusini.