Dorcus Mwakiremba: Mchezaji wa soka aliye na mkono mmoja anayetia fora Kenya

Dorcas akiwa katika mazoezi
Maelezo ya picha,

Dorcas akiwa katika mazoezi

Kabla hujafa hujaumbwa. Dorcus Kero Mwakiremba alizaliwa na mikono yake miwili miaka 31 iliyopita katika kaunti ya Taita-Taveta pwani ya Kenya lakini sasa hana mkono wake wa kushoto.

Mwaka 2014 mwezi wa tatu Dorcus alihusika kwenye ajali mbaya katika barabara ya Mombasa-Nairobi akiwa kazini.

``Lilikua gari aina ya pick-up, nami nilikua kwa dirisha lililokua wazi. Gari lilipobingirika nilitupwa nje na sikuwa nimefunga mkanda wa usalama, gari hilo likaangukia mkono wangu wa kushoto.

``Sitasahau siku hiyo. Kwa muda mfupi niliona ndoto zangu za maisha zimefifia. Nashukuru Mungu wangu sikufa.Nilikimbizwa Hospitali na baadae ikabidi mkono wangu wa kushoto ukatwe.''

Familia yake Dorcus haikuamini kabisa ana mkono mmoja tu sasa baada ya ajali hiyo. Nyumbani kwao ni Voi katika kaunti ya Taita-Taveta.

Maelezo ya picha,

Dorcas Kero alizaliwa na mikono yake miwili miaka 31 iliyopita katika kaunti ya Taita-Taveta pwani ya Kenya lakini sasa hana mkono wake wa kushoto.

``Babangu (Cleopa Mwakiremba) na mamangu (Elizabeth Mchemi) walichukua muda kukubali nilivyo. Ndugu zangu (Elijah Mnyasa na Martha Wawuda) walibubujikwa na machozi kuona hali yangu lakini nikawatulizwa nikiiwaambia ndio hali ya maisha niko sawa.''

Maelezo ya picha,

Dorcas Kero akiwa na mwanzilishi wa klabu ya kandanda ya Soccer Divas ya Mombasa, Maria Mpaata.

Mwaka jana Dorcus aliamua aanze kucheza kandanda, na akiichezea timu yake Rotaract ya Mombasa kwenye mashindano ya saratani ya matiti, alifurahisha wengi kwa ujasiri wake wa kucheza na mkono mmoja.

Mariam Mpaata, mwanzilishi wa timu ya kandanda ya Soccer Divas, hatimaye aliamua Dorcas ajiunge nao.

``Nilishangaa na kupata morali sana nilipomuona Dorcus uwanjani,'' anasema Maria, ''Ndiposa nikaamua nimchukue. Sote tumempokea kwa uzuri Soccer Divas.

``Mimi kama kipa wa Soccer Divas nikimuona Dorcus mbele yangu ninapata nguvu zaidi. Anacheza bila uoga hata sisi hatumuangalii kama mchezaji ambaye ana mkono mmoja.''

Dorcus anasema nia yake kubwa kucheza kandanda ni kuwapa binadamu wengine matumaini katika maisha, na kwamba atazidi kujihusisha na mchezo huu nia yake kubwa ikiwa ni kusafiri kote duniani kuwapa walemavu morali.

Tangu ahusike kwenye ajali hiyo, Dorcus anahimiza wasafiri wazingatie umuhimu wa kujifunga mikanda ya usalama.

``Kama siku hiyo ya ajali nilikua nimejifunga mkanda, singerushwa nje ya gari lakini imefanyika sina la kufanya.Nimekubali hali yangu nilivyo,'' asema Dorcus, mzaliwa wa pili kwa familia ya watoto watatu.