Marekani washindwa kufuzu Kombe la Dunia Urusi

Christian Pulisic Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Christian Pulisic aling'aa sana akichezea Marekani mechi za kufuzu lakini sasa atasubiri miaka minne kucheza mara ya kwanza Kombe la Dunia

Marekani hawatashiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka ujao nchini Urusi baada ya kulazwa 2-1 na Trinidad & Tobago mechi ya kufuzu kwa michuano hiyo Jumanne.

Panama waliingiza mchanga kitumbua cha Marekani kwa kuandikisha ushindi dhidi ya Costa Rica.

Vijana hao wa Bruce Arena walianza mechi wakiwa katika nafasi ya tatu ya kufuzu kwa Kombe la Dunia lakini bao la ushindi la Roman Torres dakika ya 88 liliwafikisha Panama kwa michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

Marekani hawakupata hata nafasi ya kucheza michuano ya muondoano ya kufuzu dhidi ya Australia, kwani nafasi hiyo iliwaendea Honduras waliowalaza Mexico.

Mara ya mwisho kwa Marekani kukosa kushiriki fainali za Kombe la Dunia ilikuwa mwaka 1986.

Marekani walilaza Panama 4-0 Ijumaa iliyopita lakini licha ya kucheza dhidi ya Trinidad & Tobago waliokuwa na alama tatu pekee kutoka kwa mechi tisa walizocheza awali za kufuzu, walicheza vibaya sana na hakukuwa na matumaini yao ya kushinda.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Roman Torres aliibuka shujaa wa Panama kwa kufunga dakika ya 88

Matokeo kamili mechi za Jumanne:

  • Trinidad & Tobago 2-1 USA
  • Honduras 3-2 Mexico
  • Panama2-1 Costa Rica
Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Panama wakisherehekea kufuzu