Sadio Mane: Liverpool kukaa nje ya uwanja wiki sita

Sadio Mane Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Sadio Mane alifungia Liverpool mabao 13 msimu uliopita

Mshambuliaji wa Liverpool Sadio Mane huenda akakaa nje kwa hadi wiki sita baada ya kupata jeraha la misumi ya paja akichezea Senegal mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Mane, 25, aliondolewa uwanjani dakika ya 89 mechi ambayo walilaza Cape Verde 2-0 Jumamosi.

Mchezaji huyo hataweza kucheza dhidi ya Manchester United na Tottenham na pia mechi mbili za Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Maribor.

Mane amefunga mabao matatu katika mechi tano za Ligi ya Premia alizocheza msimu huu.

Senegal, wanaongoza kundi lao la kufuzu kwa Kombe la Dunia, lakini wana mechi muhimu dhidi ya Afrika Kusini mnamo 10 na 14 Novemba, mechi ambazo kuna uwezekano huenda Mane akakosa kushiriki.

Liverpool walishinda mechi moja pekee kati ya saba katika mashindano yote Mane akiwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwezi Januari.

Mabao ya wastani waliyofunga wakiwa na Mane Ligi ya Premia ni 2.2, na bila yeye 1.6 kila mechi.

Mada zinazohusiana