Nyota wa Chelsea N'Golo Kante kukaa nje wiki tatu baada ya kuumia

N'Golo Kante Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption N'Golo Kante ameshinda Ligi ya Premia misimu miwili England - akiwa na Leicester na Chelsea

Chelsea wamesema kiungo wao wa kati N'Golo Kante hataweza kucheza kwa wiki tatu baada ya kuumia misuli ya paja akichezea timu ya taifa.

Mchezaji huyo wa miaka 26 alichechemea na kuondoka uwanjani wakati wa mechi ambayo Ufaransa walilaza Bulgaria 1-0 wikendi iliyopita.

Sasa, hataweza kucheza hadi mwezi ujao.

Meneja wa Chelsea Antonio Conte amesema kwamba mchezaji huyo atahitaji kupigwa picha mguuni na kuchunguzwa zaidi.

Kiungo wa kati mwenzake Danny Drinkwater anapiga hatua vyema katika kuuguza jeraha la misuli ya sehemu ya chini ya miguu lakini bado hayuko tayari kuchezea Chelsea mechi yake ya kwanza.

Conte hata hivyo amesema mshambuliaji Alvaro Morata atakuwa sawa kucheza dhidi ya Roma Jumatano katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Meneja huyo amesema kutokana na kukosekana kwa Kante huenda akahitajika kuchezesha baadhi ya mabeki kama viung wa kati.

David Luiz amewahi kucheza safu ya kati awali lakini Kante amesema hangependelea kumhamisha.

Chipukizi Ethan Ampadu au Kyle Scott huenda wakachezeshwa dhidi ya Crystal Palace Jumamosi.

Mada zinazohusiana