'Mwanangu amenichukia kwa sababu tuliwachapa Arsenal' - Deeney

Troy Deeney of Watford celebrates

Nahodha wa klabu ya Watford ya Uingereza amesema mwanawe alikasirishwa sana naye baada ya klabu hiyo kuwalaza Arsenal 2-1 Jumamosi.

Troy Deeney amesema nyumbani kwake "hakungekalika" wikendi kwa sababu mwanawe anaipenda sana Arsenal.

Deeney alimpongeza sana mwenzake Tom Cleverley aliyefunga bao la ushindi uwanjani Vicarage Road.

Amesema uamuzi kuwapa Watford penalti iliyozaa bao la kwanza huenda ulikuwa mkali kidogo kwa Arsenal lakini akasema hajashangaa kwamba Arsenal wamekuwa wakilalamika.

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger alikosoa saa uamuzi huo na kuutaja kuwa "uamuzi wa kashfa".

Gunners waliongoza kupitia bao la kichwa la Per Mertesacker lakini Watford walisawazisha kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Troy Neeney baada ya Hector Bellerin kudaiwa kumchezea visivyo Richarlison eneo la hatari zikiwa zimesalia dakika 19.

Deeney alikuwa ameingia uwanjani kama nguvu mpya.

Tom Cleverley alifunga bao la ushindi sekunde za mwisho za mechi na kuwawezesha Watford kupanda hadi nafasi ya nne kwenye jedwali.

"Naweza kusema hiyo haikuwa penalty," alisema Wenger. "Ilitokea wakati muhimu kwenye mechi kwa Watford. Bila penalti, hawana bao."

Watford watakutana na Chelsea uwanjani Stamford Bridge Jumamosi ijayo.

Arsenal watashuka dimbani Europa League siku ya Alhamisi ugenini kwa Red Star Belgrade nchini Serbia.