Ben Foster: Kipa wa West Brom aumia akicheza na mwanawe Uingereza

Ben Foster Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ben Foster alikuwa amechezea West brom mechi nane kabla ya kuikosa mechi hiyo ya Jumatatu

Mlinda lango wa klabu ya West Brom Ben Foster aliumia kwenye goti akicheza na mwanawe kwenye bustani nyumbani kwao, meneja wa klabu hiyo Tony Pulis amesema.

Kipa huyo alikosa mechi ambayo West Brom walitoka sare ya 1-1 na Leicester siku ya Jumatatu.

Pulis alisema wana wasiwasi sana na kwamba wanasubiri uchunguzi zaidi kubaini ubaya wa jeraha hilo la goti.

"Hatungemhatarisha zaidi uwanjani usiku wa leo," Pulis alisema baada ya mechi Jumatatu.

Foster alikaa miezi 10 bila kucheza tangu Machi 2015 baada ya kuumia kano za goti.

"Alikuwa anacheza na mwanawe wa kiume kwenye bustani nyuma ya nyumba yao na alipinda goti kidogo na kwa sababu ana tatizo na kano za goti tuna wasiwasi," Pulis aliongeza.

Kipa Boaz Myhill alijaza nafasi ya Foster uwanjani King Power na alimtia Pulis wasiwasi zaidi baada ya kugongana na mshambuliaji wa Leicester Jamie Vardy kipindi cha pili.

Hata hivyo alicheza hadi mwisho.

Kipa huyo mwingine wa West Brom ni Alex Palmer, 21, ambaye hana uzoefu wa ligi kuu.

Mada zinazohusiana