Cavani aokoa Paris St-Germain baada ya Neymar kula kadi nyekundu

Edinson Cavani

Edinson Cavani alifunga bao dakika ya 93 kupitia mkwaju wa ikabu na kuwawezesha Paris St-Germain kutoka sare na Marseille baada ya Neymar kufukuzwa uwanjani.

Luiz Gustavo alikuwa amefunga bao la kwanza mechi hiyo na kuwaweka Marseille kifua mbele kipindi cha kwanza lakini Neymar akakomboa kwa bao lake la 10 tangu ahamie PSG kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika.

Florian Thauvin aliwarejesha Marseille mbele zikiwa zimesalia dakika 10 kabla ya Neymar kupewa kadi mbili za manjano katika kipindi cha dakika mbili na kufukuzwa uwanjani.

Cavani kisha alisawazisha kwa kombora la hatua 25 kutoka kwenye goli ambalo liliugonga mwamba wa goli kisha likaingia kimiani.

Maelezo ya picha,

Neymar alikuwa amefunga bao lake la 10 tangu ahamie PSG

Mbrazil huyo aliyehamia PSG kutoka Barcelona kwa rekodi ya dunia ya £200m, alipewa kadi ya pili dakika ya 87 baada yake kukorofishana na Lucas Ocampos, aliyeanguka mbele ya mwamuzi.

PSG hawajashindwa mechi yoyote msimu huu na wamo alama nne mbele ya Monaco kileleni Ligue 1.

Marseille wamesalia nafasi ya tano.