Ronald Koeman: Everton wamfuta kazi meneja baada ya kushindwa na Arsenal

Ronald Koeman

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Ronald Koeman aliteulwia meneja wa Everton kabla ya msimu wa 2016-17

Klabu ya Everton imemfuta kazi meneja Ronald Koeman baada ya kichapo cha 5-2 Jumapili kutoka wka Arsenal kuwaacha wakiwa kwenye eneo la kushushwa daraja kwenye jedwali Ligi ya Premia.

Taarifa ya klabu hiyo imemshukuru Ronald kwa huduma alizotoa kwa klabu hiyo katika kipindi cha miezi 16 iliyopita.

Everton wamo nafasi ya 18 Ligi Kuu England na wameshinda mechi mbili pekee kati ya tisa walizocheza ligini msimu huu.

"Bado naamini ninaweza kubadili hali hii," Koeman alikuwa amesema Jumapili.

Koeman amekuwa meneja wa tatu Ligi ya Premia kufutwa msimu huu baada ya Frank de Boerwa Crystal Palace na Craig Shakespeare wa Leicester.

Mholanzi huyo wa miaka 54 alikuwa amewasaidia Everton kumaliza nafasi ya saba msimu wake wa kwanza lakini msimu huu mambo yameenda mrama licha ya kutumia £140m sokoni majira ya joto.

Uwezekano wao kusonga kutoka Kundi E Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ni finyu baada ya kushindwa na Atalanta na Lyon na kutoka sare na Apollon Limassol.

Koeman alikuwa amefika uwanjani Finch Farm kwa mazoezi leo asubuhi wakijiandaa kwa mechi ya Jumatano katika Kombe la Carabao dhidi ya Chelsea.

Lakini mwenyekiti Bill Kenwright na afisa mkuu mtendaji Robert Elstone walifika bila kutarajiwa na baadaye kufutwa kwake kukatangazwa.