UEFA: Man U yaichapa Benfica 2-0

Kwa mara ya mwisho Daley Blind kufunga goli ilikuwa Desemba 2016
Image caption Kwa mara ya mwisho Daley Blind kufunga goli ilikuwa Desemba 2016

Manchester United ikiwa nyumbani katika dimba la Old Trafford imefanikiwa kuichapa Benfica 2-0 na kwa mara ya kwanza ndani ya miaka minne inaweza kuingia katika hatua ya mtoano.

United ambayo imeingia katika mashindano hayo kwa kuchukua kikombe cha ligi ya Europa msimu uliopita wameshinda michezo yote minne waliocheza na hivyo wanahitaji alama moja pekee katika michezo miwili iliyosalia ili kuweza kufuzu moja kwa moja.

Anthony Martial, ambaye alikuwa tishio katika mchezo huo, alikosa mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa katika eneo la hatari na Douglas na mkwaju wake kuchezwa na mlinda mlango wa Benfica Mile Svilar ambaye alikuwa katika kiwango kizuri.

Image caption Licha ya kushindwa kufunga mkwaju wa penalti, Antony Martial alionyesha kiwango bora

Svilar aliokoa pia mikwaju miwili mikali ya Mbelgiji mwenzake Romelu Lukaku kabla ya kujifunga goli la kwanza baada ya mkwaju mkali wa Nemanja Matic kumgonga mgongoni.

Marcos Rashford aliyeingia kipindi cha pili aliongeza mashambulizi zaidi kwa upande wa Manchester United na kusababisha penalti ambayo ilifungwa vyema na Daley Blind.

Benfica ilionyesha kiwango kizuri lakini mlinda mlango wa Man U David de Gea aliokoa mikwaju yao yote.

Kwa matokeo hayo Man U inaongoza ikiwa na alama 12, huku Benfica ikiburuta mkia na alama 0.