Roma yaicharaza Chelsea 3-0 vilabu bingwa

Wachezaji wa Chelsea wakiwa wamewachwa vinywa wazi baada ya kuzabwa mabao 3 bila jibu na Roma

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Wachezaji wa Chelsea wakiwa wamewachwa vinywa wazi baada ya kuzabwa mabao 3 bila jibu na Roma

Chelsea imekuwa timu ya kwanza katika ligi ya Uingereza kupoteza mechi ya vilabu bingwa msimu huu baada ya kushindwa na Roma ilioimarika.

The Blues ingesonga mbele iwapo ingeibuka mshindi lakini ikajipata nyuma katika sekunde 39 baada ya Edin Dzeko kumgusia pasi nzuri El Sharaawy aliyecheka na wavu kufuatia krosi iliopigwa na Aleksander Kolarov.

Alvaro Morata alikosa nafasi nzuri kusawazisha akiwa katika eneo hatari , kabla ya El Sharaawy kuiweka kifua mbele Roma baada ya beki wa zamani wa timu hiyo Antonio Rudiger kukosa kuondoa mpira uliokuwa umepigwa katika lango la Chelsea.

Chelsea Ilifanya mashambulio mengi lakini walikuwa chini 3-0 wakati Diego Perotti alipofunga kutoka maguu 20 baada ya beki wa Chelsea kushindwa kumkaba.

Roma karibu ifanye mambo kuwa 4-0 wakati mabeki wa Chelsea walipomkimbilia Dzeko ambaye alimpigia pasi murua Perroti lakini mshambuliaji huyo akapiga juu badala ya kucheka na wavu.

Hatahivyo Chelsea walibahatika baada ya Atletico Madrid kushindwa kuilaza Qarabag baada ya mechi hiyo kumalizika 1-1 hatua inayoiwezesha timu hiyo kuwa katika nafasi nzuri ya kufuzu katika mechi za muondoano.