Conte hajui hatima ya David Luiz Chelsea

David Luiz

Chanzo cha picha, Rex Features

Meneja wa Chelsea Antonio Conte amesema hafahamu iwapo beki David Luiz atasalia Stamford Bridge.

Mchezaji huyo wa miaka 30 hakujumuishwa kwenye kikosi cha Chelsea dhidi ya Manchester United Jumapili na hata hakuwekwa kwenye benchi.

Badala yake, meneja huyo alimchezesha Andreas Christensen.

Alipoulizwa kumhusu Luiz, Conte alisema: "Lazima atie bidii la sivyo atakuwa kwenye benchi au kwenye viti vya mashabiki."

Kuhusu mustakabali wa Luiz, Conte aliongeza: "Sijui, Christensen ndiye sasa na siku za usoni kwa Chelsea."

Mbrazil Luiz amecheza dakika 90 katika kila mechi za Chelsea tatu walizokuwa wamecheza karibuni Ligi ya Premia na alicheza walipolazwa 3-0 na Roma Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katikati ya wiki.

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha,

David Luiz alikaa nyuma ya benchi wakati wa mechi dhidi ya Manchester United

Lakini Jumapili, aliketi nyuma ya benchi ya Chelsea, akiwa amejifunga skafu ya rangi nyeusi kichwani.

Alirejea mara ya pili Chelsea kwa £34m kutoka Paris St-Germain Agostit 2016 na alikuwa kwenye kikosi kilichoshinda ligi msimu uliopita.