Andrea Pirlo: Nyota wa Italia atangaza kustaafu soka

Andrea Pirlo

Kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Italia Andrea Pirlo ametangaza kustaafu uchezaji soka baada ya kuchez mechi yake ya mwisho kalbu ya New York City.

Mchezaji huyo wa miaka 38 alichezea Italia mechi 116 na aliwasaidia kushinda Kombe la Dunia mwaka 2006.

Pirlo alianza uchezaji wake Brescia na alichezea Inter, AC Milan na Juventus kabla ya kujiunga na Ligi Kuu ya Soka Amerika Kaskazini (MLS) miaka miwili iliyopita.

"Sio tu kwamba muda wangu hapa New York umefikia kikomo bali pia safari yangu kama mchezaji soka pia imefika tamati," amesema.

Kwenye taarifa kwenye akaunti yake ya Twitter, Pirlo pia ameshukuru "kila timu ambayo nilipata heshima ya kuchezea" na "kila mchezaji ambaye nimebahatika kucheza naye".

Klabu yake ya zamani Juventus imemweleza kama "jagina halisi".

Meneja wa klabu ya New York City Patrick Vieira amesema Pirlo "alibadilisha soka daima".

Pamoja na kuwasaidia Azzurri kuwa mabingwa wa dunia, Pirlo alishinda mataji mengi ya soka nchini mwake katika miaka 22 aliyocheza soka.

Alikuwa kwenye kikosi cha Milan kilichoshinda mataji mawili ya Serie A, vikombe viwili vya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na Kombe la Dunia la Klabu kati ya 2003 na 2011, na kisha akachangia sana ushindi wa Juventus wa ligi mara nne kati ya 2012 na 2015.

Alihamia New York kabla ya kuanza kwa msimu wa MLS wa mwaka 2015 na kujiunga na kiungo wa kati wa zamani wa England Frank Lampard ana mshambuliaji wa zamani wa Uhispania David Villa katika klabu hiyo inayomilikiwa na Manchester City.

Alisaidia klabu hiyo ambayo mkufunzi wake ni Patrick Vieira kufika mechi za muondoano kutafuta bingwa misimu miwili iliyopita, lakini hakuweza kushinda vikombe akiwa nao.

Maelezo ya picha,

Pirlo alicheza mechi ya mwisho kama nguvu mpya dakika ya 90 'dhidi ya Columbus Crew

Uchezaji wa Pirlo kwa tarakimu

Mechi 872

Mataji ya Serie A 6

Coppa Italia 2

Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya 2

Kombe la Dunia 1

Maelezo ya picha,

New York City FC wameshukuru kiungo huyo wao wa kati

Maelezo ya picha,

AC Milan pia wamemtakia heri Pirlo

Maelezo ya picha,

Juventus wamemshukuru mchezaji huyo aliyewasaidia kushinda vikombe saba misimu minne

Maelezo ya picha,

Mshambuliaji wa zamani wa England Gary Lineker pia amemsifu Pirlo kwa ufanisi wake