Naby Keita: Mchezaji aliye na matumaini makubwa

Naby Keita

Naby Keita huenda alianza msimu wa 2016-17 kama mchezaji asiye na umaarufu nchini Ujerumani, lakini alikamilisha msimu huo jina lake likiwa katika kikosi cha timu ya mwaka - kura iliopigwa ambapo mchezaji huyo wa Guinea alipata kura nyingi kushinda kiungo wa kati yeyote yule.

Klabu ya Red Bull Leipzig ndiyo iliowashangaza wengi katika msimu wa 2016-17, huku ikimaliza katika nafasi ya pili (na kufuzu katika mashindano ya vilabu bingwa), lakini ilikuwa kiungo huyo wa kati aliyeisadia timu hiyo kuwa katika nafasi ya pili.

Dakika tano tu baada ya kuchezeshwa katika kikosi cha kuanza mechi mara ya kwanza katika Bundesliga, Keita aliyenunuliwa kutoka klabu dada cha Red Bull Salzburg ya Austria, alifunga bao la ushindi dhidi ya Borussia Dortmund kunako dakika ya 89 na hivyo basi kushinda taji la mchezaji bora na timu bora ya msimu.

Kwa jumla, alifunga mabao manane, mojawapo likiwa bao lililoorodheshwa kuwania tuzo ya bao bora la msimu huku akitoa usaidizi katika ufungaji wa mabao 7.

Mchezaji huyo pia anapendwa sana kwa uwezo wake wa kurudi nyuma na kulinda lango.

Ni uchezaji kamilifu wa Keita kwa jumla unaowafurahisha mashabiki wa soka.

Ni kiungo wa kati ambaye ni hatari katika sehemu yoyote ya uwanja, 'wachezaji wa upinzani wakimtaja kuwa ''wachezaji wawili''.

Huwezi kusikiliza tena
Naby Keita: Mchezaji aliyewavutia sana Liverpool

Keita, mwenye miguu yenye kasi, ni mchezaji ambye makocha wengi wangependa kuwa naye.

Keita ana nguvu na akili ya kuwapangua na pia kuwapiga chenga wapinzani na kisha maono ya kuweza kufanikisha mashambulizi na kufunga mabao au kusaidia kuyafunga.

Aliweza kutamba na kugeresha mpira zaidi ya winga wa Bayern Arjen Robben katika msimu uliopita wa ligi ya Bundesliga.

Ndio sababu mkufunzi wake katika klabu ya Leipzig Ralph Hasenhutt amemtaja kuwa kiungo muhimu kwa kipaji chake kisichokuwa cha kawaida.

Nyota huyo aliyezaliwa mjini Conakry aliwavutia wengi na kuilazimu Liverpool kuweka uhamisho uliovunja rekodi kwa wachezaji wa kutoka barani Afrika wa £48m ili kupata huduma zake kuanzia mwezi Julai 2018. Huku Leipzig wakisema kuwa wasingemuuza bali ni kulingana na sheria ya uhamisho.

Keita yuko katika orodha hii ya wachezaji kwa sababu ya mchango wake kwenye klabu kwani Guinea haikufanikiwa kufuzu katika Kombe la Dunia la Urusi 2018, licha ya kiungo huyo kufunga mabao katika mechi za kufuzu kwa kombe hilo dhidi ya Libya na Tunisia.

Anasema kuwa anamuenzi na anafuata nyayo za Yaya Toure. Je, kiungo huyo atamuiga raia huyo wa Ivory Coast na kujishindia tuzo ya mchezaji bora wa Afrika ya BBC kwa mwaka 2017?

Mada zinazohusiana