Victor Moses: Hatimaye ametulia na kutamba Chelsea

Victor Moses

Victor Moses atakapotafakari kuhsuu maisha yake ya uchezaji, kuna uwezekano mkubwa kwamba kiungo huyo wa kati wa Nigeria na Chelsea atautazama msimu wa 2016-17 kama wakati ambao nyota ya jaha ilimuangazia.

Baada ya miaka kadhaa ya kutanga jangwani akiwa anatumwa nje kwa mkopo mara kwa mara, mchezaji huyo wa miaka 26 hatimaye alitia guu na kutulia Stamford Bridge, sana kiasi kwamba alitekeleza mchango muhimu katika kikosi kilichoshinda Ligi ya Premia.

Siku ambayo Moses ataikumbuka ni 1 Oktoba baada ya kocha wa Chelsea Antonio Conte baada ya vipigo vikali mfululizo kutoka kwa Arseanal na Liverpool alipobadili mfumo na kucheza 3-4-3 na kiungo huyu raia wa Nigeria akachezeshwa kwenye nafasi asiyoizoea pembezoni kwenye winga ya kulia kwenye mchezo dhidi ya Hull City.

Ulikuwa mchezo wake wa kwanza ligi kwake kuanza kwenye kikosi akiichezea Chelsea kwa karibu miaka mitatu. Lakini Moses alikuwa mchezaji bora na aliichangamkia sana fursa hiyo na kuonyesha mchezo wake wa kushambulia na pia kuwa mkabaji hali ikilazimu.

Ushindi dhidi ya Hull ulikuwa mwanzo wa ushindi mara 13 mfululizo kwa Chelsea kwenye ligi kuu nchini Uingereza na ukawa ni mchezo wa 22 wa Moses kuanza kwenye kikosi ligini mtawalia, hadi alipotupwa nje na jeraha kwa muda mwezi Aprili.

Mwezi uliotangulia, mchezaji huyo wa Nigeria alikuwa amejitolea maisha yake ya usoni kwa kutia saini mkataba mpya - na kukamilisha mabadiliko makubwa ya hali yake klabu hiyo tangu alipojiunga nao mara ya kwanza 2012.

Ingawa hili sana lilitokana na Conte kumpenda Moses baada ya kuona kitu ambacho wengine walikuwa hawajakiona kwake wakati wa kujiandaa kwa msimu, mchezaji huyo wa miaka 26 bado alihitaji kudhihirisha uwezo wake.

Huwezi kusikiliza tena
Victor Moses: Mchezaji aliyewavusha Nigeria hadi Urusi

Katika moja ya hadithi ambazo hazikutarajiwa msimu huo, alidhihirisha uwezo wake na hata zaidi kwa nguvu zake, ustadi wake akicheza na kasi yake.

"Mkataba huu mpya ni ishara ya bidii na kujitolea kwa Victor kutaka kufanikiwa," alimsifia mkurugenzi wa kiufundi wa Chelsea aliyeondoka majuzi Michael Emenalo.

Hatimaye aliibuka na kuwa mshindi wa Ligi ya Premia na pia akajitwalia medali ya fedha (mshindi wa pili) baada ya Chelsea kushindwa kwenye fainali ya Kombe la FA ambapo Moses alitia doa uchezaji wake msimu huo kwa kupata kadi nyekundu.

Moses amecheza michezo mitatu ya kimataifa pekee mwaka huu lakini katika mechi yake ya kwanza alifunga bao na kuchangia ushindi mkubwa wa timu yake wa 4-0 dhidi ya Cameroon, ushindi uliowaondoa mabingwa hao wa Afrika kutoka kwa kinyang'anyiro cha kfuuzu kwa Kombe la Dunia na kulainisha njia ya Nigeria hatimaye kufuzu kwa michuano hiyo kwa mara ya tatu.

Baaada ya kuwasaidia Super Eagles kufika nchi ya ahadi, je Moses anaweza kuwa Mnigeria wa kwanza kutwaa tuzo ya BBC baaada ya Jay-Jay Okocha kutwaa tuzo hiyo mwaka 2014?