Kombe la Dunia: Nigeria yachukua hatua kuzuia mzozo na wachezaji Urusi

Nigeria captain John Mikel Obi (left) in action against Argentina Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Nahodha wa Nigeria John Mikel Obi alikuwa kwenye kikosi cha wachezaji waliozozana na serikali kuhusu malipo mwaka 2013 wakati wa Kombe la Mabara Brazil

Shirikisho la soka Nigeria (NFF) na wachezaji wa taifa hilo wamesaini mkataba kuhusu malipo watakayopokea watakaposhiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018.

Rais wa shirikisho hilo Amaju Pinnick amesema atajitahidi kuepukana na shida ambazo zimezikumba timu za Afrika ambazo zimeshiriki michuano ya Kombe la Dunia miaka iliyopita.

Nahodha wa timu hiyo John Mikel Obi ameukaribisha mkataba huo.

''Tunafurahia na kukaribisha maendeleo haya,'' alisema Mikel.

''Hii ni mara ya kwanza tangu nilipoanza kuchezea timu kuu ya taifa kwamba naona kila kitu kuhusu maandalizi, bonasi na marupurupu vyote vinaandikwa kwa wino na mkataba kutiwa saini.

''Inatutuliza moyo kwamba sasa tuna viongozi kwenye shirikisho ambao wamejitolea kuhakikisha kila kitu kinatekelezwa ndio maana walipanga mkutano huu na kuwaruhusu wachezaji kushiriki na saini mkataba huo.''

Mkataba huo, unaohusisha jinsi malipo yatakavyokuwa na kiwango kamili, ulitiwa saini baada ya mkutano kati ya wachezaji wenye na viongozi wakuu wa NFF kabla ya mechi ya Jumanne ambayo waliandikisha ushindi wa magoli 4-2 mechi ya kirafiki dhidi ya Argentina katika mji wa Urusi wa Krasnodar.

Naibu rais wa NFF Shehu Dikko amesema mkataba huo ni nakala iliyo na mambo yote muhimu ikijumuisha pia mechi za kujiandaa kwa michuano ya nchini Urusi.

Mataifa mengine kutoka Afrika pia ambayo yamekumbana na shida za marupurupu na usumbufu wakati wa michuano ya Kombe la Dunia ni Ghana, Cameroon na Togo.

Mada zinazohusiana