Peter Crouch aongeza mkataba Stoke

Peter Crouch Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Peter Crouch amesema anaamini anaweza kuendelea kucheza Ligi ya Premia hadi atimize miaka 40

Mshambuliaji wa klabu ya Stoke Peter Crouch ametia saini mkataba mwingine wa mwaka mmoja katika klabu hiyo, hatua itakayomuweka katika klabu hiyo hadi 2019.

Crouch, 36, ambaye amechezea England mechi 42, ndiye mfungaji mabao bora wa klabu hiyo ambapo amewafungia mabao manne msimu huu.

Hii ni licha ya kwamba mechi tisa ambazo amewachezea Ligi ya Premia msimu huu ameingia kama nguvu mpya.

"Bado ana mchango muhimu wa kutekeleza kwetu," meneja Mark Hughes amesema.

Crouch alijiunga na Stoke kutoka Tottenham mwaka 2011 kwa uhamisho wa £10m uliovunja rekodi ya klabu hiyo wakati huo.

Awali, alikuwa amechezea Liverpool, Portsmouth, QPR, Southampton na Aston Villa.

Mapema mwezi huu, aliweka rekodi Ligi ya Premia kwa kuingia mara nyingi zaidi kama nguvu mpya - mara 143 baada ya kuingia kama nguvu mpya dhidi ya Brighton.

Oktoba, alitambuliwa pia kama mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwa kichwa Ligi ya Premia, mabao 51.

Mada zinazohusiana