Pep Guardiola: Meneja wa Man City ajutia kumzungumzia Nathan Redmond wa Southampton

Guardiola approaches Redmond Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Guardiola baadaye alisema alikuwa anamsifia Redmond

Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amesema anajutia sana mazungumzo ambayo alifanya na mchezaji wa Southampton Nathan Redmond punde baada ya mechi yao kumalizika Jumatano.

City walishinda 2-1.

Guardiola, ambaye aliingia uwanjani na kuzungumza na winga huyo, ametakiwa kufafanua kuhusu kitendo hicho chake na Chama cha Soka cha England.

Redmond amesema Mhispania huyo alikuwa tu anamsifia.

Ijumaa, Guardiola alisema: "Siwezi kujidhibiti. Natumai nitaweza kufanya hivyo, natumai naweza kuimarika."

Meneja huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich amepewa hadi Jumatatu kutoa ufafanuzi.

"Kile Redmond alichosema ndicho hicho, navutiwa naye kama mchezaji na namshukuru kwa aliyoyasema," amesema.

"Iwapo FA wanataka taarifa yangu tena, ninaweza kufafanua chochote wanachotaka nifafanue. Ikiwa hawaniamini, sijui nafanya nini hapa."

Guardiola alimwendea Redmond muda baada ya Raheem Sterling kufunga bao la ushindi la City dakika ya 96 uwanjani Etihad.

Alianza kusema kwa sauti na kuashiria kwa mikono yake, huku Redmond akionekana kufunika mdomo wake na kumjibu.

Redmond baadaye amesema: "Nilimwambia kwamba nilikuwa ninafanya kile nilichoambiwa na meneja wangu kufanya kwenye mechi hiyo. Hivyo tu."

City watakuwa wenyeji wa West Ham saa 16:00 GMT Jumapili nao Southampton watakuwa ugenini dhidi ya Bournemouth saa 13:30 siku hiyo.

Mada zinazohusiana