Golikipa anusuru klabu iliyoweka rekodi ya aibu Italia

Benevento celebrate Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Gennaro Gattuso (kulia) alikuwa anawaongoza Milan kwa mara ya kwanza

Mlindalango wa kalbu ya Benevento Alberto Brignoli alifunga bao la kusawazisha dakika za mwisho kwenye mechi na kuiwezesha klabu yake kutoka sare ya 2-2 na AC Milan Jumapili.

Matokeo hayo yaliiwezesha klabu hiyo kupata alama yake ya kwanza katika Ligi Kuu ya Italia Serie A katika historia yao.

Klabu hiyo ilikuwa imeweka rekodi ya kupoteza mechi nyingi zaidi mwanzo wa msimu zaidi ya timu nyingine yoyote katika moja ya ligi kuu tano Ulaya.

Rekodi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Manchester United.

Golikipa huyo, ambaye yuko nao kwa mkopo kutoka Juventus, alifunga bao kwa kichwa baada ya frikiki iliyopigwa na Danilo Cataldi.

Aliwawezesha kufikisha kikomo mkimbio wa kushindwa mechi 14 mfululizo.

Milan walikuwa wanaongoza kupitia bao la Giacomo Bonaventura kabla ya George Puscas kusawazisha.

Nikola Kalinic aliwaweka Milan mbele tena na mchezaji wao Alessio Romagnoli alioneshwa kadi nyekundu baadaye kabla ya Brignoli kufunga bao la ushindi.

"Nina furaha sana sio kwangu mimi pekee bali kwa sababu ya kila mtu," Brignoli alisema baada ya mechi.

"Tumepoteza mechi nyingi sana kwa mabao ambayo hatukustahili kufungwa dakika ya 90, sasa ni wakati wetu kusherehekea."

Milan, ambao walishuka hadi nafasi ya nane, walikuwa wanacheza mechi yao ya kwanza chini ya Gennaro Gattuso baada ya kumfuta meneja wao Vincenzo Montella.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Alberto Brignoli alikuwa anacheza mechi ya Serie A mara yake ya tisa

Benevento ambao ndio mara ya kwanza wanacheza Serie A - walikuwa wanacheza ligi ya daraja la tatu msimu wa 2015-16.

Brignoli ndiye kipa wa kwanza kufunga bao Serie A tangu Massimo Taibi alipowafungia Reggina dhidi ya Udinese mwaka 2001.

Haki miliki ya picha EPA

Mada zinazohusiana