Mwamuzi ashindwa penalti itapigiwa wapi Ujerumani

Cologne Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mechi ilicheleweshwa dakika 30 ili theluji iondolewe

Itakuwaje ukiwa mwamuzi na uamue penalti inafaa kupigwa lakini ukose eneo ambalo huwa la kupigiwa mikwaju hiyo?

Hilo lilifanyika katika mechi moja ya Ligi Kuu Ujerumani, Bundesliga, kati ya Cologne na Freiburg Jumapili.

Maeneo mengi Ulaya yamekuwa yakishuhudia kuanguka kwa theluji kwa kiwango cha juu majira haya ya baridi.

Mwamuzi Robert Kampka alikuwa na wakati mgumu mshambuliaji wa Cologne Sehrou Guirassy alipochezewa visivyo dakika 18 ya mechi.

Uwanja ulikuwa umejaa theluji kabla ya mechi kuanza na ilibidi watu kuitwa kuiondoa. Mechi ilicheleweshwa kwa dakika 30.

Mistari kwenye uwanja ilichorwa tena kabla ya mechi kuanza, lakini yamkini walisahau kuweka alama eneo la kupigiwa penalti.

Wakati huo Cologne, ambao hawajashinda mechi hata moja ligini msimu huu, walikuwa wanaongoza kupitia goli la Lukas Klunter.

Kampka alipoamua Cologne wapige penalti, yeye na wachezaji wa Cologne hawakuweza kujua mkwaju huo ungepigiwa wapi.

Mwamuzi huyo alilazimika kupima hatua 11 kutoka kwenye mstari wa goli, kuamua eneo la mita 11 kutoka kwenye goli ambapo mkwaju huo ungepigiwa.

Guirassy alifunga na kufanya mambo kuwa 2-0.

Caleb Stanko alijifunga na klabu hiyo ikawa inaongoza kwa 3-0, kabla ya mambo kuwageuka.

Nils Petersen na Janik Haberer walifungia Freiburg mawili kabla ya Petersen kufunga penalti dakika ya 90 na nyingine tena muda wa ziada na kuwashindia mechi hiyo.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Sehrou Guirassy alifunga penalti

Mabao yake matatu yaliwafanya Freiburg, ambao walikuwa wa pili kutoka mkia, kuwa alama 12 juu ya Cologne.

Wakati Petersen akipiga mikwaju yake, theluji ilikuwa imeachwa kuanguka uwanjani.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Mistari ilichorwa upya kwa rangi nyekundu uwanjani baada ya theluji kuondolewa
Haki miliki ya picha Reuters
Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Hali ya uwanja ilikuwa imeimarika pakubwa Nils Petersen alipopiga mikwaju yake miwili ya penalti

Mada zinazohusiana