Mabondia wanne akiwemo Fatuma Zarika wapewa tuzo ya heshima na Rais Kenyatta

Fatuma Zarika akikabiliana na Belinda Laracuente wa Puerto Rico katika pigano la kutetea ubingwa wa dunia upande wa wanawake uzani wa feather. Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Fatuma Zarika (kushoto) akikabiliana na Belinda Laracuente wa Puerto Rico awali

Bingwa wa dunia uzani wa super-bantam chama cha WBC Fatuma Zarika na Rayton Okwiri ni miongoni mwa mabondia wanne wa Kenya wa kulipwa ambao Jumanne wiki hii wamepata tuzo ya heshima kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta kuadhimisha siku kuu ya Jamhuri.

Mabondia hao wanne wamepata tuzo inayojulikana kama Head of State Commendation (HSC).

Mbali na Zarika na Okwiri, wengine waliopata tuzo hiyo ni Maurice Okolla na James Onyango ambaye hivi majuzi alishinda taji la World Boxing Organisation (WBO) uzani wa welter kwa kumshinda Saidi Mundi wa Tanzania katika hoteli ya Carnivore jijini Nairobi.

Wakati Onyango akimshinda Mundi, Zarika naye siku hiyo hiyo alihifadhi taji lake la dunia kwa kumshinda kwa pointi Catherine Phiri wa Zambia katika pigano la raundi kumi uzani wa super-bantam, naye Okwiri akamshinda kwa pointi bondia mwingine wa Tanzania Imani Daudi.

Zarika, mwenye umri wa miaka 32, alitwaa mkanda huo mwaka jana huko Michigan, Marekani, kwa kumshinda kwa pointi Alicia Ashley wa Jamaica. Hii ilikua ni mara ya kwanza anatetea ubingwa wake wa dunia dhidi ya Phiri.

Kwa matokeo hayo Zarika ameshinda mapigano 30, akapoteza mara 12 na kwenda sare mara mbili.

Haki miliki ya picha HISANI
Image caption Zarika akiwa na bondia mstaafu Mike Tyson nchini Marekani

Miongoni mwa mapigano hayo 30 aliyoshinda, 17 ni kwa knockout.

Zarika alijiunga na ndondi mwaka wa 2000 mtaa wa Mathare jijini Nairobi, akashinda mapigano matatu na akapoteza mara moja katika ndondi za ridhaa. Laila Ali, bintiye bondia mashuhuri duniani Muhammad Ali, ndiye alichangia sana Zarika kujifunza ndondi.

"Nilivutiwa sana na vile alikua anacheza nilipomtizama kwenye TV nami nikaamua nataka niwe kama Laila,'' anasema Zarika.

Mwaka wa 2011 aliamua kucheza ndondi za kulipwa, na miongoni mwa mabondia alioshinda hapo mwanzo ni Rukken Koronoso wa Afrika Kusini na Esther Herkole.

Mada zinazohusiana