Pep Guardiola: 'Poleni Manchester United - lakini si Mourinho'

Manchester City manager Pep Guardiola (left) and Manchester United counterpart Jose Mourinho

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

City waliweka mwanya wa alama 11 kileleni Ligi ya Premia kati yao na United walipowalaza Jumapili

Meneja wa klabu ya Manchester City Pep Guardiola amesema anaomba radhi kwa Manchester United iwapo sherehe za City baada ya kuwashinda mahasimu hao wao wa jiji ziliwakera.

Hata hivyo, amesema hawezi kuomba radhi eti kwa sababu Jose Mourinho alikereka.

Mourinho alirushiwa maziwa nje ya chumba cha kubadilishia mavazi baada yake kwenda kulalamikia jinsi City walivyokuwa wakisherehekea baada ya kushinda debi ya Manchester Jumapili.

"Iwapo tuliwakera United - sio mchezaji mmoja, au Jose - Manchester United, basi naomba radhi," amesema Mhispania huyo.

Mourinho amesema matukio hayo baada ya ushindi wa City wa 2-1 yalikuwa "tofauti ya kitabia, na kielimu".

Kisha, alikamilisha kikao chake na wanahabari Jumanne kwa kudokeza kwamba kuendelea kuangaziwa kwa matukio hayo kunaashiria kutowaonea heshima Bournemouth, ambao watacheza dhidi ya United baadaye Jumatano.

Chama cha Soka cha England kimezipatia klabu hizo mbili za Manchester hadi Jumatano kujibu kuhusu yaliyotokea wakati huo.

Hata hivyo Guardiola amesema wachezaji wana haki ya kusherehekea, hasa baada ya ushindi huo kuwafanya kuwa alama 11 mbele ya United.

"Ni lazima tufurahie haya. Iwapo watu hawaelewi, basi pole. Tulishinda debi," alisema.

"Iwapo hatukuwa sahihi, basi nawaomba radhi Manchester United. Nia yetu haikuwa hiyo. Nia yetu ilikuwa kusherehekea ndani ya chumba cha kubadilishia mavazi."

Uhasama

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mourinho alikimbia uwanjani Nou Camp kusherehekea baada ya Inter Milan kuwalaza Barcelona nusufainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya 2010

Mourinho na Guardiola walifanya kazi pamoja Barcelona, Mourinho akiwa msaidizi wa wakufunzi na Pep mchezaji, lakini uhusiano wao umedorora.

Alipoondoka Chelsea 2007, Mourinho anadaiwa kuhojiwa na wakuu wa Barcelona kuhusu kazi ya umeneja lakini badala yake Guardiola ambaye hakuwa na uzoefu mwingi kama yeye akapewa kazi hiyo Frank Rijkaard alipoondoka.

Miaka miwili baadaye, Mourinho alikimbia uwanjani Nou Camp kusherehekea baada ya Inter Milan kuwalaza Barcelona nusufainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya 2010. Guardiola alibaki kushangaa.

Akiwa Real Madrid, Mourinho alimwelekezea kidole jichoni msaidizi wa Guardiola Tito Vilanova na kudokeza kwamba Barca walikuwa wanapendelewa na waamuzi na maafisa wa Uefa.

Guardiola alipoondoka Barca na kuchukua likizo kutoka kwa soka 2012, Mourinho alisema ni hatua ambayo "haiwezi kufikirika".

"Yeye ni mdogo wangu, lakini mimi sijachoka," alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Guardiola akisherehekea na wachezaji wake Jumapili

Guardiola naye amesema kuwa anapotazama na kuzipima timu zinazosimamiwa na Mourinho huwa hataki kujifunza kutoka kwa 'vituko' vya Mourinho pembeni mwa uwanja.

Wote wawili walipewa kazi Manchester majira ya joto 2016 na walikutana mara tatu msimu uliopita, City wakashinda ligini Old Trafford Septemba, United wakashinda Old Trafford mechi ya Kombe la Ligi na mechi ya ligi ya Etihad Aprili ikaisha kwa sare tasa.

Kabla ya mechi ya Jumapili, Mourinho alidokeza kwamba wachezaji wa City hujiangusha na kufanya makosa ya kiufundi ili kufaidi kwenye mechi.