Conte: Ukweli usemwe kuhusu Manchester City EPL

Chelsea's Tiemoue Bakayoko celebrates scoring against Huddersfield
Maelezo ya picha,

Tiemoue Bakayoko alifunga dhidi ya Huddersfield

Meneja wa klabu ya Chelsea Antonio Conte ametetea tamko lake kwamba Chelsea hawana matumaini ya kushinda Ligi Kuu ya England msimu huu.

Amesema hayo hata baada ya Chelsea kujikwamua kutoka kwa kichapo mikononi mwa West Ham na kulaza Huddersfield Town 3-1 Jumanne.

Ushindi wao uliwafanya kutoshana kwa alama na Manchester United walio nafasi ya pili ingawa wako nyuma kwa mabao.

Mabao ya Chelsea yalifungwa na Tiemoue Bakayoko, Willian na Pedro.

Chelsea bado wamo alama 11 nyuma ya viongozi Manchester City, pengo ambalo Conte anaamini haliwezi kuzibwa.

"Lazima ukubali uhalisia. Napendelea kusema ukweli badala ya kusema uongo," alisema Conte baada ya mechi ya jana.

"Wakati mwingine naweza kuwa muwazi kupita kiasi lakini huwa napenda kuzungumza kwa uwazi na wachezaji wangu na mashabiki wetu. Haimaanishi kwamba tumeacha kujaribu kuwafikia (City).

"Njia yetu ni njia nzuri, lakini kwa kweli kuna timu ambayo ipo mbele yetu. Ni vigumu sana, sasa, kuwazuia."

Maelezo ya picha,

Chelsea walipata ushindi wao wa kwanza ugenini Ligi ya Premia tangu 18 Novemba

Maelezo ya picha,

Ni Manchester City, Manchester Untied na Liverpool pekee ambao wamefunga mabao mengi kuliko Chelsea Ligi ya Premia msimu huu

Chelsea kwenye mechi hiyo pia walimchezesha kinda wa miaka 17, Ethan Ampadu, kama nguvu mpya, mara yake ya kwanza kuchezeshwa kwenye timu kubwa, mechi ikiwa imesalia dakika kumi.

Aliibuka mchezaji wa pili mdogo zaidi kwa umri kuchezeshwa Ligi ya Premia na Chelsea baada ya Jody Morris mwaka 1996.

Maelezo ya picha,

Chelsea walifaidi sana kutokana na uwepo wa Willian

Huddersfield watakutana na Watford ugenini Jumamosi, nao Chelsea wawe nyumbani dhidi ya Southampton siku hiyo Ligi ya Premia.