Mourinho: Ningekuwa likizoni Brazil ningejua hakuna njia ya kuwazuia Manchester City

Manchester United celebrate

Chanzo cha picha, Getty Images

Meneja wa klabu ya Manchester United Jose Mourinho amesema "angelikuwa likizoni Brazil au Los Angeles" iwapo angekuwa anaamini kwamba mbio za Ligi ya Premia msimu huu zimepata mshindi.

Alisema hayo baada ya klabu yake kulaza Bournemouth 1-0 Jumatano.

United walijikwamua kutoka wka kichapo cha Manchester City wikendi lakini hawakuweza kupunguza mwanya kati yao na City ambao wamo alama 11 mbele yao kwani vijana hao wa Etihad walilaza Swansea 4-0.

Romelu Lukaku ndiye aliyewafungia Man United bao hilo la ushindi kipindi cha kwanza.

Mourinho alisema: "Mechi hiyo dhidi ya City ilikuwa kubwa, na ukishindwa hilo halisaidii juhudi zako za kujiweka sawa tena - ushindi husaidia, kushindwa hakusaidii.

"Bournemouth walikuwa wapinzani wakali na hali ilikuwa ngumu. Kama tungelifunga bao la pili tungetulia.

"Nimefurahishwa na alama hizo tatu. Walipumzika siku moja zaidi yetu, walikuwa sawa kutushinda baada ya kupumzika, hata kiakili kwa sababu mechi kubwa huwadhoofisha wachezaji zaidi.

"[Mbio za ligi] zitamalizika tu Mei. Kama zingekuwa zimemalizika sasa ningeenda likizo Brazil au Los Angeles."

Msimamo wa Mourinho ni tofauti na meneja wa Chelsea Antonio Conte ambaye amekiri kwamba itakuwa vigumu kuwazuia Manchester City.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Beki wa Manchester United Luke Shaw alianza mechi kwa mara ya kwanza ligini msimu huu

United walikuwa wamecheza mechi 40 nyumbani bila kushindwa hadi walipolazwa na vijana hao wa Pep Guardiola Jumapili.