Zanzibar wafuzu kwa fainali Cecafa baada ya kuilaza Uganda

Nahodha wa Zanzibar Suleiman Kassim
Image caption Nahodha wa Zanzibar Suleiman Kassim

Zanzibar wamefuzu kwa fainali ya ubingwa wa kanda ya Afrika mashariki na kati, maarufu kama Cecafa Senior Challenge baada ya kuwalaza Uganda Cranes 2-1.

Zanzibar Heroes sasa watakutana na Kenya kwenye fainali Jumapili.

Zanzibar walifunga mwanzo kupitia Abdul Azizi Makame dakika ya 25 kisha Derrick Nsibambi akatuliza kimiyani bao la Uganda la kusawazisha naye Mohammed Issa Juma akapachika wavuni bao la pili la Zanzibar .

Ni mara ya kwanza kwa Zanzibar kufika fainali michuano hiyo tangu 1995, mwaka ambao walitwaa ubingwa.

Allan Katerega wa Uganda anasema kuondolewa kwa Joseph Nsubuga kuliipunguzia nguvu timu yao.

Nsubuga alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Feisal Salum Abdulla wa Zanzibar.

Image caption Mchezaji wa Uganda Allan Katerega

Wenyeji Kenya walifuzu baada ya kuwashinda Burundi kwa bao la muda wa ziada lililofungwa na kiungo wa kati Whyvonne Isuza.

Katibu mtendaji wa baraza la taifa la michezo Zanzibar Khamis Ali Mzee tayari amesema: "Sasa Fifa wapende wasipende watatutambua."

Image caption Bw Khamis Ali

Zanzibar si wanachama wa Fifa licha ya kupigana kwa muda mrefu watambuliwe.

Wanajumuishwa wote pamoja na Tanzania bara.

Lakini Ali asema ndugu mkubwa hawapi fungu lao kutoka Fifa.

"Nitasema hapo tumefinywa lakini tutafanikiwa siku moja."

Image caption Wachezaji wa Uganda wakirejea uwanjani kwa kipindi cha pili

CAF pia haitambui chama cha kandanda cha Zanzibar.

Huwezi kusikiliza tena
Hemed: Wachezaji wa Zanzibar katika Cecafa hawana doa

"Walijaribu kutuzuia CAF tusishiriki michuano hii ya Cecafa lakini ndugu mkubwa akatutetea tena tuliwaambia sisi ni baadhi ya waanzilishi miaka hiyo ikiwa Gossage Cup," asema Ali.