Kaka: Nyota wa zamani wa Brazil na AC Milan atangaza kustaafu

Kaka Haki miliki ya picha Getty Images

Kiungo wa kati wa zamani wa AC Milan na Real Madrid Kaka ametangaza kustaafu soka.

Kaka alishinda Kombe la Dunia mwaka 2002 akiwa an Brazil.

Mchezaji huyo wa miaka 35 alianza uchezaji soka wake Brazil akiwa na klabu ya Sao Paulo, na amekuwa akichezea Orlando City inayocheza Ligi Kuu ya Amerika ya Kaskazini (MLS).

Kaka alicheza mechi yake ya mwisho Oktoba Orlando walipomaliza msimu, na mwezi Novemba taarifa zilisema alikuwa amepewa kazi ya kuwa mkurugenzi katika klabu ya AC Milan.

Yeye ni miongoni mwa wachezaji wanane pekee waliowahi kushinda Kombe la Dunia, Kombe la Ulaya/Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na tuzo ya Ballon d'Or.

Wengine ni Bobby Charlton, Gerd Muller, Franz Beckenbauer, Paolo Rossi, Zinedine Zidane, Rivaldo na Ronaldinho.

Kaka alichezea Brazil mechi 92 na kuwafungia mabao 29.

Baada ya kushinda Kombe la Dunia, alishinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa na Milan mwaka 2007 na akakabidhiwa tuzo ya Ballon d'Or (tuzo ya mchezaji bora duniani) mwaka huo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kaka alirejea AC Milan kwa matembezi Novemba

Aling'aa zaidi miaka sita aliyokuwepo Italia kati ya 2003 na 2009 ambapo alishinda taji la Serie A mwaka 2004 na Kombe la Dunia la Klabu 2007.

Baada ya kuhamia Madrid kwa uhamisho uliovunja rekodi ya dunia wa £56m Juni 2009, Kaka alishinda Copa del Rey 2011, na mwaka uliofuata akashinda La Liga.

Baadaye alitatizwa na majeraha ya goti na akarejea Milan kwa msimu mmoja 2013 kabla ya kuelekea Orlando mwaka uliofuata.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii