Zanzibar sasa yaomba kutambuliwa na Fifa

Maelfu na maelfu ya mashabiki walimiminika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume kuwapongeza mashujaa wao waliotetemesha miamba katika mashindano hayo
Image caption Maelfu na maelfu ya mashabiki walimiminika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume kuwapongeza mashujaa wao waliotetemesha miamba katika mashindano hayo

Wachezaji wa Zanzibar walilakiwa kwa shangwe na hoi hoi walipotua nyumbani kutoka Kenya baada ya kumaliza wa pili katika mashindano ya kandanda ya kombe la Cecafa Senior Challenge kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati.

Maelfu na maelfu ya mashabiki walimiminika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume kuwapongeza mashujaa wao waliotetemesha miamba katika mashindano hayo, miongoni mwao wakiwa ni Tanzania bara, Uganda na Kenya.

Katika mechi za mchujo Zanzibar iliicharaza Tanzania kwa bao 1-0, matokeo ambayo hayakuwafurahisha mashabiki na viongozi wa mpira wa miguu nchini humo ikikumbukwa kwamba Zanzibar ingali inapigania kuwa huru kwa chama chake kutambuliwa na shirikisho linalosimamia kandanda duniani, Fifa.

``Matokeo yetu ya kufana katika mashindano ya Cecafa ni ujumbe tosha kwa Fifa kwamba tuko tayari kujitawala kimpira,'' asema katibu mtendaji wa baraza la taifa la michezo Zanzibar Khamis Ali Mzee ambaye aliongoza kikosi cha Zanzibar nchini Kenya.

Image caption Fifa ingali bado haitambua chama cha kandanda cha Zanzibar (ZFA), sababu yao kubwa wanasema kisiwa cha Zanzibar ni nchi moja na Tanzania ndiposa wanatambua TFF.

``Ni wakati mzuri sasa Fifa itambue ZFA kwa sababu tumeonyesha dunia nzima tuna talanta kwenye kandanda, na tukijitawala wenyewe basi tutapiga hatua kubwa zaidi ya wenzetu wa Tanzania bara. Kama Scotland na Wales, kwa mfano, ni wanachama wa Fifa mbona nasi pia tusitambuliwe?''.

Fifa ingali bado haitambua chama cha kandanda cha Zanzibar (ZFA), sababu yao kubwa wanasema kisiwa cha Zanzibar ni nchi moja na Tanzania ndiposa wanatambua TFF.

``Sisi hatuna chuki na wenzetu wa Tanzania bara ila twataka Fifa itutambue,'' asema kocha wa Zanzibar Heroes Hemed Suleiman akieleza hawapati fungu lolote kutoka Fifa kwa sababu pesa zote inapokea TFF.

``Kile tumefaidika nacho kutoka TFF kufikia sasa ni uwanja wa nyasi bandia peke yake,'' ana sema Khamis Ali.

Katika mechi ya fainali Zanzibar ilisimama wima na kwenda sare na Kenya mabao 2-2 baada ya muda wa ziada lakini hatimaye wenyeji walibeba kombe kwa mabao 3-2 ya penalti. Katika mechi za nusu-fainali, Zanzibar ilishinda Uganda Cranes kwa mabao 2-1 na Kenya ikailaza Burundi bao 1-0 la muda wa ziada.

Image caption Hata kipa nyota wa zamani wa timu ya Kenya, Mahmoud Abbas, hakufarahishwa na mchezo wa Kenya licha ya kubeba kombe.

Kwa jumla Zanzibar walionyesha mpira mzuri wa kasi na chenga fupi fupi zilizowapa shida kubwa wachezaji wa Kenya. Kwa vyovyote vile Zanzibar ilistahili kushinda mashindano hayo kwani walicheza vizuri zaidi ya Kenya ambao walisuasua tu bila kuonyesha mchezo wa kufana.

Hata kipa nyota wa zamani wa timu ya Kenya, Mahmoud Abbas, hakufarahishwa na mchezo wa Kenya licha ya kubeba kombe.

``Hatuna timu kabisa hapa, ni ubabaishaji mwingi,'' Abbas aliambia BBC Swahili mjini Kisumu Kenya ilipojikokota na kushinda Burundi bao 1-0 mechi ya nusu fainali.

``Siku hizi huwezi jua nani yuko timu ya taifa ya Kenya kwa sababu wachezaji wanabadilishwa kila mara. Siku zetu haikua hivyo. Nilichezea timu ya taifa kwa zaidi ya miaka kumi nikiwa pamoja na wenzangu Hussein Kheri, Peter Otieno ``Bassanga'', John ``Bobby'' Ogolla, Josphat Murila, Sammy Taabu, Joe Masiga, Wilberforce Mulamba, Ambrose Ayoyi na wengine wengi.''

Image caption Baadhi ya watumbuizaji waliofika katika uwanja wa ndege kuilaki timu hiyo ya Zanzibar

Abbas anasema kocha mpya Paul Put atalazimika kutembea kote nchini kutafuta wachezaji wapya waiongeze nguvu timu ya taifa, na kwamba matumaini yao ya kufuzu kwa fainali ya kombe la mataifa ya Afrika mwaka wa 2019 nchini Cameroon ni haba.

Mada zinazohusiana