Gabriel Jesus: Mshambuliaji wa Manchester City kukaa nje mwezi mmoja

Gabriel Jesus aliondoka uwanjani akitokwa na machozi baada ya kuumia kipindi cha kwanza Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Gabriel Jesus aliondoka uwanjani akitokwa na machozi baada ya kuumia kipindi cha kwanza

Mshambuliaji nyota wa Manchester City Gabriel Jesus atakuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya mwezi mmoja kutokana na jeraha alilopata wakati wa mechi dhidi ya Crystal Palace Jumapili ambapo walitoka sare 0-0, meneja Pep Guardiola amesema.

Mbrazil huyo wa miaka 20 alionekana kuumia kwenye goti kipindi cha kwanza wakati wa mechi hiyo uwanjani Selhurst Park.

Aliondolewa uwanjani akitokwa na machozi.

Kiungo wao Kevin de Bruyne pia huenda akakosa kuwachezea kwa muda baada ya kuondoka uwanjani akiwa amebebwa kwa machela.

Mbelgiji huyo hata hivyo alionekana nje ya uwanja baada ya mechi, dalili kwamba huenda hakuumia sana.

"Nafikiri Gabriel atakuwa nje kwa mwezi mmoja hivi au siku chache zaidi, naye Kevin tutasubiri Jumatatu tujue iwapo aligongwa tu kidogo au ameumia sana," alisema Guardiola.

"Ni lazima ukubali ukali na ugumu wa ukabaji Ligi ya Premia, lakini waamuzi wanahitaji kuwalinda wachezaji, hilo ndilo naomba pekee."

Jesus atakosa mechi dhidi ya Watford Jumane.

De Bruyne naye ambaye ameng'aa sana msimu huu na kusaidia ufungaji wa mabao tisa Ligi ya Premia msimu huu aliumia baada ya kukabiliwa na kiungo wa Palace Jason Puncheon.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kevin de Bruyne alikabwa na Jason Puncheon

"Kuna mstari ambao unapouvuka inakuwa hatari," amesema Guardiola.

Palace walifikisha kikomo mkimbio wa kushinda mechi 18 wa City, lakini walivuka mwaka wakiwa na alama 14 mbele kileleni.

Sergio Aguero ndiye mshambuliaji wao pekee aliye sawa, lakini Guardiola amekataa kuthibitisha taarifa kwamba wanapanga kumnunua mshambuliaji wa Arsenal Alexis Sanchez Januari.

Mada zinazohusiana