Jose Mourinho: Meneja wa Man Utd asema Paul Scholes kazi yake ni kukosoa tu

Manchester United manager Jose Mourinho Haki miliki ya picha Getty Images

Jose Mourinho amemshutumu nyota wa zamani wa Manchester United Paul Scholes baada yake kumkosoa mara kwa mara kiungo wa kati kutoka Ufaransa Paul Pogba.

Akizungumza baada ya sare ya 0-0 kati ya klabu hiyo na Southampton Jumamosi, Scholes alisema: "Haonekani kama mchezaji ambaye atakusaidia kushinda mechi - mchezaji kama huyo ndiye unafaa kutoa £90m mfukoni kwa sababu yake."

Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Everton Jumatatu, Mourinho alisema: "Jambo pekee analofanya Scholes ni kukosoa tu.

"Scholes atakumbukwa kwenye historia kama mchezaji stadi. Si kama mchambuzi mahiri wa soka.

Ufanisi wa United wakiwa na Pogba kwenye ligi
Ni siku 435 sasa tangu Paul Pogba alipomaliza kwenye timu ambayo ilishindwa mechi Ligi ya Premia akiwa na United (23 Oktoba 2016 v Chelsea). Tangu wakati huo, amecheza mechi 34 (Kushinda 21 Sare 13 Kushindwa 0), ilhali United wameshindwa mechi tano bila yeye kipindi hicho

Tamko la Scholes mwishoni mwa wiki alilitoa baada ya United kutoka sare mechi ya tatu mtawalia.

Mchezaji huyo wa zamani wa England ambaye sasa ana miaka 43 amekuwa akifanya kazi kama mchambuzi katika runinga ya BT Sport na alikosoa mtazamo wa Pogba na kudokeza kwamba huenda pia hayuko sawa kimwili kucheza.

Haki miliki ya picha Rex Features and BBC

"'Anazurura' tu wakati wa mechi," alisema Scholes.

"Pogba haonekani kuwa sawa kucheza, nashangaa iwapo anafanya mazoezi vyema.

"Hakuna yeyote England anafaa kuwa akifika karibu naye, lakini anatakiwa kufanya majukumu ambayo hapendezwi nayo.

"Inabidi useme kwamba meneja anafaa kulaumiwa kwa hilo."

Pogba, 24, alicheza zaidi safu ya mashambulizi dhidi ya Everton zaidi ya alivyocheza dhidi ya Southampton, na alisaidia mabao yaliyofungwa na Anthony Martial na Jesse Lingard waliposhinda 2-0.

Mourinho alisema: "Sifikiri yeye (Shcoles) huwa anatoa maoni. Yeye hukosoa - ambalo ni jambo tofauti.

"Si kila mtu anaweza kuwa stadi kama alivyokuwa. Alipokuwa mchezaji alikuwa hodari ajabu, lakini haina maana kwamba sote twafaa kuwa kama yeye.

"Wakati mwingine Pogba hucheza vyema, wakati mwingine hucheza vyema na wakati mwingine huwa hachezi vyema. Pogba hutia bidii kila wakati.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Pogba alisaidia ufungaji wa mabao yote mawili dhidi ya Everton

"Si kosa lake Paul kwamba ameunda pesa nyingi zaidi ya Paul Scholes. Si kosa la Paul Pogba, ni vile tu soka ilivyo."

Mourinho aliongeza pia kwamba iwapo Scholes atakuwa meneja siku moja, "ningependa sana awe na ufanisi angalau 25% ya ufanisi wangu."

Mada zinazohusiana