Pep Guardiola: Meneja wa Man City asema mpangilio wa mechi umekuwa balaa England

Kevin de Bruyne was carried off at Crystal Palace Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kevin de Bruyne, ambaye amesaidia ufungaji wa mabao mengi zaidi ligini msimu huu aliumia akicheza dhidi ya Crystal Palace

Meneja wa viranja wa Ligi ya Premia Manchester City Pep Guardiola amesema mpangilio wa mechi nyingi msimu wa sikukuu umekuwa "janga" kwa wachezaji.

City, ambao wamo alama 12 mbele ligini, wakiwa na mechi moja hawajacheza, watakutana na Watford Jumanne, ambayo itakuwa mechi yao ya nne katika siku 11 msimu wa Krismasi na Mwaka Mpya.

Wachezaji wao muhimu Gabriel Jesus na Kevin de Bruyne waliumia wakati wa mechi dhidi ya Crystal Palace Jumapili.

Mhispania huyo alisema: "Iwapo utaniambia kwamba kiufundi, kimwili inawafaa wachezaji: la hasha, ni janga."

Jesus aliandika Jumatatu kwamba anaona heri kidogo kwamba hatahitaji kufanyiwa upasuaji.

Mkimbio wa City wa kushinda mechi 18 mtawalia ulifikishwa kikomo walipotoka sare Selhurst Park ikiwa ni mara yao ya kwanza kushindwa kufunga kwenye mechi ligini msimu huu.

Ikizingatiwa kwamba amekuwa mkufunzi Uhispania na Ujerumani ambapo kipindi hicho timu hupumzika, Guardiola alisema imemlazimu kuzoea utamaduni wa Uingereza.

Haki miliki ya picha Getty Images

Guardiola amewahimiza waamuzi "kuwalinda" wachezaji dhidi ya kukabwa vikali.

Alikuwa amedokeza kwamba anatarajia Jesus atakuwa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja au zaidi kidogo.

Ubaya wa jeraha la De Bruyne bado haujabainika.

Mada zinazohusiana