Scott Dann na Jason Puncheon: Wachezaji wa Crystal Palace waliomkabili Kevin de Bruyne hawatacheza tena msimu huu

Scott Dann and Kevin de Bruyne Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Dann na Puncheon wote waliumia wakimkabili Kevin de Bruyne

Wachezaji wawili wa Crystal Palace Scott Dann na Jason Puncheon hawatacheza tena msimu huu baada yao kuumia sana kwenye kano za goti wakimkabili mchezaji nyota wa Manchester City Kevin de Bruyne, meneja wao Roy Hodgson amesema.

Dann ambaye ni nahodha aliondolewa uwanjani kwa machela wakati wa mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa sare tasa Jumapili.

Palace walifikisha kikomo mkimbio wa City wa kushinda mechi 18 mfululizo.

Puncheon aliumia alipomkabili De Bruyne dakika ya mwisho ya mechi.

"Hatutawaona tena uwanjani msimu huu na huenda wasiwe tayari kucheza mwanzo wa msimu ujao," amesema Hodgson.

"Wote watamtembelea mtaalamu na kuna uwezekano watafanyiwa upasuaji magoti yao yatakapoacha kuvimba. Ni majeraha mabaya sana."

Dann na Puncheon wote wawili walipewa kadi za manjano kwa kumchezea visivyo De Bruyne.

Dann, 30, kutoka alimkaba Mbelgiji huyo nje ya eneo la hatari naye Puncheon, 31, alifika kuzuia City wasijibu shambulizi baada ya mkwaju wa penalti wa dakika za lala salama wa Luka Milivojevic kuokolewa na Ederson.

De Bruyne alipata nafuu na aliweza kuanza kwenye kikosi cha City kilichowalaza Watford 3-1 Jumanne.

Palace nao walifanikiwa kutoka nyuma na kulaza Southhampton 2-1 siku hiyo.

Hodgson alisema kabla ya mechi hiyo kuanza kwamba ana wasiwasi sana kutokana na majeraha kikosi chake na kwamba mechi nyingi msimu wa Krismasi zilikuwa mzigo kwa wachezaji wake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii