Moyes amhurumia Alan Pardew baada ya West Ham kuwalaza West Bromwich Albion

Andy Carroll Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Andy Carroll alikuwa hajafunga bao lolote katika mechi 12 alizokuwa amecheza karibuni zaidi

Meneja wa West Ham David Moyes alisema anamhurumia sana mwenzake wa West Brom Alan Pardew kuhusu mpangilio wa mechi za klabu hiyo.

Alisema hayo baada ya West Ham kupata ushindi wa dakika za mwisho dhidi ya West Brom.

West Brom walikuwa wanacheza mechi yao ya pili katika siku tatu na walijiweka kifua mbele kupitia kombora la James McClean.

Lakini Andy Carroll alifunga mawili, la pili akilifunga dakika ya 94 na kuwaondoa West Ham eneo la kushushwa daraja Liig ya Premia.

West Brom walikuwa wameomba mechi hiyo ya Jumanne iahirishwe ikizingatiwa kwamba ilikuwa inacheza siku mbili tu baada yao kucheza dhidi ya Arsenal.

West Ham upande wao walikuwa hawajacheza mechi yoyote tangu 26 Desemba.

"Iwapo ningelikuwa Alan Pardew ningesikitishwa sana na jinsi Ligi ya Premia wamepanga mechi hizi," alisema Moyes.

"Hungedhani kwamba ndiyo timu iliyokuwa imecheza mechi siku mbili zilizopita."

West Brom hawajashinda mechi hata moja kati ya nane walizocheza tangu Pardew alipoteuliwa meneja Novemba na alifikiri vijana wake walitatizwa na uchovu wa kimwili na kiakili.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Andy Carroll amechezea timu ya taifa ya England mechi tisa tangu, mara ya mwisho 2012.

Mada zinazohusiana