Jose Mourinho: Taarifa kwamba nitaondoka Manchester United ni 'takataka'

Jose Mourinho Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Jose Mourinho ameeleza wazi kwamba United wanahitaji kutumia pesa zaidi

Jose Mourinho amesema uvumi kwamba anapanga kuondoka Manchester United mwisho wa msimu ni taarifa zisizo na maana au takataka.

Mourinho kwa sasa anaendelea na mazungumzo na klabu hiyo kuhusu mkataba mpya lakini kuna taarifa kwamba hajafurahishwa na mambo Old Trafford na anapanga kuondoka.

Kujitolea kwake kusalia katika klabu hiyo kumeongezwa shaka na hali kwamba ameendelea kuishi hotelini badala ya kuishi katika nyumba yake.

"Nasema ni takataka. Siwezi kupata maneno mazuri ya kuelezea taarifa hizo," Mourinho amesema.

"Jambo baya zaidi mtu anaweza kufanya ni kuonesha chembe ya shaka katika utaalamu wangu, kwa kila kitu kuhusu kazi yangu, kwa hivyo ndio taarifa hizo zisizo na maana zimenigusa kwa hili kwa sababu ni jambo ambalo siwezi kukiri.

"Narudia, nipo katikati ya mazungumzo kuhusu mkataba wangu, kutia saini mkataba mpya kwangu kutegemea klabu lakini kujitolea kwangu ni kamili na ningependa kusalia."

Mourinho mkataba wake wa sasa unafikia kikomo mwaka 2019.

Taarifa zinasema mazungumzo ya kina yamefanyika kati ya naibu mwenyekiti mtendaji wa United Ed Woodward na washauri wa Mourinho kuhusu uwezekano wake kuendelea kusalia Old Trafford.

"Najiona nikiwa hapa bado," aliongeza Mourinho.

"Ni swali tu la klabu, bodi na wamiliki, Bw Woodward, wote wana furaha kuhusu mchango wangu na wangependa niendelee hata baada ya kumalizika kwa mkataba wa sasa."

Mreno huyo pia amezungumzia kinachodaiwa kuwa kupoteza hamu kwake United.

"Kwa sababu tu sijifanyi kama mwanasarakasi uwanjani? Hiyo ina maana kwamba nimepoteza motisha?" alisema mkufunzi huyo wa miaka 54.

"Huwa napenda kufanya mambo kwa njia yangu, kwa ukomavu zaidi, njia bora zaidi kwa timu na mimi mwenyewe, si lazima ujifanye kama mtu mwendawazimu uwanjani.

Mourinho alisema kujitolea kwa mtu kazini hakuwezi kuoneshwa na "anachofanya akiwa mbele ya kamera".

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii