Everton kumchukua mshambuliaji wa Besiktas Cenk Tosun kwa £27m

Cenk Tosun Haki miliki ya picha Getty Images

Everton wamekubaliana na klabu ya Besiktas ya Uturuki kuhusu kumnunua mshambuliaji Cenk Tosun.

Meneja wa Everton Sam Allardyce amesema kilichosalia sasa ni makubaliano kati ya klabu na mchezaji huyo.

Everton walifanya mkutano na rais wa Besiktas Fikret Orman Jumatano kuhusu uhamisho ambao unatarajiwa kuwa wa £27m.

Tosun, 26, amekuwa London akisubiri idhini ya kukamilisha uhamisho huo.

Allardyce amesema anatumai Tosun atasajiliwa kwa wakati kumuwezesha kucheza dhidi ya Liverpool katika raundi ya tatu ya Kombe la FA Ijumaa.

Tosun aliwasaidia Besiktas kufika hatua ya 16 bora Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, ambapo watakutana na Bayern Munich.

Allardyce anatarajia mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Uturuki ambaye ni mzaliwa wa Ujerumani atazalisha magoli Everton baada ya klabu hiyo kukaukiwa na mabao baada ya Romelu Lukaku kuhamia Manchester United kwa £90m.

Tosun ndiye mchezaji wa kwanza kununuliwa na Allardyce tangu kuondoka kwa Ronald Koeman.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Cenk Tosun amefunga mabao manane mechi 24 alizochezea Uturuki

Mada zinazohusiana