Philippe Coutinho atambulishwa kwa mashabiki wa Barcelona Nou Camp

Philippe Coutinho Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Philippe Coutinho alitia saini mkataba Barcelona Jumatatu

Uhamisho wa Philippe Coutinho wa £142m kujiunga na Barcelona ulithibitishwa Jumatatu baada ya mchezaji huyo kutambulishwa rasmi kwa mashabiki Nou Camp.

Mbrazil huyo wa miaka 25 alitia saini mkataba akiwa pamoja na rais wa klabu hiyo Josep Maria Bartomeu, kabla ya kutambulishwa rasmi kwa mashabiki.

Liverpool na Barca waliafikiana kuhusu uhamisho wa Coutinho Jumamosi.

"Ningependa kumshukuru rais na kila mtu aliyechangia kufanikisha hili," amesema Coutinho.

"Nina furaha sana, ni ndoto ambayo imetimia na natumai kwamba nitafanya kazi yangu vyema uwanjani."

Bartomeu ameongeza: "Mashabiki wote wa Barca wana furaha kumuona Coutinho hapa."

Coutinho alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na ingawa alibainika kwamba ana jeraha paja la kulia, alikamilisha uhamisho wake.

Jeraha hilo lilimzuia kucheza mechi ambayo Liverpool walilaza Burnley 2-1 siku ya mwaka Mpya.

Barcelona wamesema kiungo huyo wa kati huenda akakaa nje wiki tatu hivi.

Hii inaashiria kwamba anaweza kutarajiwa kucheza debi ya Catalona dhidi ya Espanyol tarehe 4 Februari.

Mada zinazohusiana