Antonio Conte: Sitasahau mzozo wangu na Mourinho

Antonio Conte Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Meneja wa Chelsea Antonio Conte

Meneja wa Chelsea Antonio Conte amesema 'hatausahau' mzozo ambao alikuwa nao na meneja wa Manchester United, Jose Mourinho akiongeza kwamba hiyo ni shida miongoni mwao hao wawili na sio kwa klabu hizo.

Mourinho aliendelea kumtupia Conte maneno siku ya Jumamosi kwa kusema yeye hawezi "kupigwa marufuku yoyote kwa kosa la kupanga matokeo ya mechi", ambapo awali alikuwa amezungumzia kuhusu "mchekeshaji" uwanjani.

Mwitaliano huyo alijibu matamshi ya Mourinho kwa kumuita mtu ''mdogo.''

"Alitumia maneno makali,'' Conte aliongeza kwenye mkutano wake na wanahabari siku ya Junanne.

''Sitasahau hili.''

Conte amesema hajutii kusema ''Huyu ni mtu mdogo'' kwenye matamshi yake na hakuna sababu yoyote kwa Chama cha Mameneja wa Ligi ya Premia kuingilia kati.

"Hii si shida kutoka kwa klabu, ni shida kati yetu sisi. Nimenyamaza,'' aliongeza.

Conte alipigwa marufuku ya miezi minne akiwa meneja wa Juventus msimu wa mwaka 2012-13 kwa kukosa kuripoti kuhusu kupangwa kwa matokeo ya mechi alipokuwa katika klabu ya Siena.

Mwaka 2016 aliondolewa makosa na mahakama.

Matamshi ya Mourinho kuhusu tuhuma za kupanga matokeo ya mechi aliyatoa baada ya Conte kudai kwamba Mourinho amesahau vituko vyake vya awali.

Conte alikuwa amekerwa na tamko la Mourinho kwamba haikuwa na haja kwake kujifanya "mcheshi" au mwanamazingaombwe uwanjani ndipo aonyeshe kwamba anajitolea katika klabu yake.

"Nafikiri anastahili kujiangalia yeye mwenyewe miaka iliyopita, labda alikuwa akijizungumzia yeye mwenyewe," alisema Conte.

Mada zinazohusiana