Refa aliyempiga teke mchezaji asimamishwa kazi Ufaransa

Referee Tony Chapron Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mbrazil Diego Carlos akifukuzwa uwanjani na Tony Chapron

Refa ambaye anadaiwa kumrushia teke mchezaji wa klabu ya Nantes nchini Ufaransa kabla ya kumfukuza uwanjani mechi yao dhidi ya Paris St-Germain amesimamishwa kazi.

Chama cha Soka cha Ufaransa kimetangaza kwamba amesimamishwa kazi kwa muda usiojulikana "hadi uamuzi mwingine utolewe."

Beki Diego Carlos alimgonga mwamuzi Tony Chapron kwenye kisigino katika kilichoonekana kama ajali tu dakika za mwisho za mechi.

Chapron alimrushia teke mchezaji huyo na kisha akampa kadi ya pili ya njano, kwa sababu ya kulalamika.

PSG walishinda mechi hiyo 1-0.

Nantes wanataka kadi hiyo ibatilishwe kwani isipobatilishwa atakosa mechi moja.

FA ya Ufaransa imesema chama cha waamuzi kimeamua "kumuondoa Tony Chapron ambaye alikuwa ameteuliwa kusimamia mechi ya Ligue 1 Jumatano kati ya Angers na Troyes, hadi wakati mwingine".

Wameongeza: "Bw Tony Chapron karibuni ataitwa kukutana na kamati ya nidhamu ya LFP [Wasimamizi wa Ligi Ufaransa].

"Bw Tony Chapron, baada ya kutazama picha na video baadaye, alikiri kwamba aliangushwa kimakosa."

Haki miliki ya picha BT Sport
Image caption Refa Tony Chapron alionekana kumrushia tene Diego Carlos

Mwenyekiti wa Nantes Waldemar Kita amesema Chapron anafaa kupigwa marufuku kwa miezi sita kwa sababu ya uamuzi huo wenye utata.

Ameongeza kuwa: "Sitaki kuamini kwamba alifanya hivyo makusudi."

"Ni mzaha," Kita aliambia runinga moja ya Ufaransa.

"Nimepokea arafa 20 kutoka pande mbalimbali duniani kuniambia kwamba huyu mwamuzi ni mzaha tu.

"Nikizungumzia hili sana, nitaitwa kujibu maswali na kamati ya maadili. Hatuna haki ya kusema chochote."

Mada zinazohusiana