Wenger athibitisha Arsenal wanamtafuta Pierre-Emerick Aubameyang

Aubameyang Haki miliki ya picha Getty Images

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amethibitisha kwamba klabu hiyo inataka kumnunua mchezaji wa Borussia Dortmund mzaliwa wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang .

Wenger amewaambia wanahabari Uingereza kwamba mazungumzo yanaendelea kati ya Gunners na klabu hiyo ya Bundesliga.

Wanahabari walimwuliza Wenger iwapo ana imani kwamba watafanikiwa kumnunua mshambuliaji huyo ambaye amekuwa akitafutwa na klabu nyingi.

Aliwajibu: "Kuwa na imani au kutokuwa na imani, sijui. Kwa sasa, hatujakaribia kutia saini mkataba wowote, iwe ni kumhusu Aubameyang au mtu mwingine yeyote. Huwezi ukajua umekaribia (kumchukua mchezaji) kiasi gani."

Wenger alikuwa anazungumza na wanahabari Jumanne kabla ya mechi ya Kombe la Ligi (Carabao) Jumatano dhidi ya Chelsea.

Aubameyang, 28, ni stadi sana kwa kufunga mabao na mwandishi wa BBC Stanley Kwenda anasema bila shaka anaweza kufaa klabu hiyo ya England ambayo msimu huu imetatizika kufunga mabao.

Kufikia sasa msimu huu Aubameyang amefunga mabao 13 katika mechi 15 alizocheza.

Alifunga mabao 31 katika mechi 32 msimu uliopita na kwa sasa amepungukiwa na mabao mawili pekee kufikisha mabao 100 aliyoyafunga tangu atue Ujerumani mwaka 2013.

Duru Ujerumani zinasema itawagharimu Arsenal zaidi ya £50m kumtoa mchezaji huyo Borussia Dortmund wakifanikiwa.

Ijumaa wiki iliyopita, mkurugenzi wa michezo wa Dortmund Michael Zorc alisema Wenger aliwakosea heshima kwa kuzungumza hadharani kumhusu mchezaji huyo.

Wenger alisema nyota huyo wa Gabon anaweza "kuingia sawa" katika klabu ya Arsenal.

Klabu hizo zinaendelea na mazungumzo ambayo huenda yakaifanya Arsenal kuvunja rekodi yake ya ununuzi wa wachezaji, ambayo inashikiliwa na ununuzi wa Alexandre Lacazette kwa £46.5m.

Kando na uchezaji, Aubameyang anafahamika sana pia kwa utukutu wake.

Ameachwa nje ya kikosi cha Dortmund mara mbili msimu huu kutokana na utovu wa nidhamu.

Hakurudi kucheza kikosini Ijumaa kama ilivyotarajiwa klabu yake ilipotoka sare ya 1-1 na Hertha Berlin.

Kwa mujibu wa mwandishi wa michezo wa BBC David Ornstein, Arsenal wana imani kwamba watafikia makubaliano katika kipindi cha wiki moja ijayo kuhusu ada ya uhamisho wake na kwamba huenda wakamtoa mchezaji mmoja wao.

Arsenal wakifanikiwa kumchukua Aubameyang, basi huenda wasiwanunue wachezaji wengine kipindi hiki.

Walikuwa miongoni mwa klabu zilizokuwa zinashindania kumnunua beki wa West Brom Jonny Evans.

Mada zinazohusiana