Usain Bolt Bolt afanya mazoezi na Mamelodi Sundowns

Usain Bolt

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Usain Bolt alifanya mazoezi na Mamelodi Sundowns Jumatatu

Binadamu mwenye kasi zaidi duniani, raia wa Jamaica Usain Bolt, alijiunga na klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mazoezi katika uwanja wao wa mazoezi wa Chloorkop Jumatatu.

Mwanariadha huyo wa miaka 31 ambaye ameshinda dhahabu Olimpiki mara nane na ndiye anayeshikilia rekodi za dunia za mbio za 100m na 200m yumo ziarani nchini humo kama sehemu ya mpango wa serikali ya Afrika Kusini wa kuimarisha riadha nchini humo.

Mabingwa hao wa soka Afrika wa mwaka 2016 walitangaza kuwasili kwa Bolt kupitia Twitter na kupakia video ya Mjamaica huyo akifanya mazoezi na wachezaji.

Bolt alistaafu kutoka kwenye riadha Agosti mwaka jana baada ya mashindano ya ubingwa wa dunia jijini London.

Mwanariadha huyo ni shabiki sugu wa klabu ya Manchester United ya Uingereza na amekuwa akizungumzia hamu yake ya kutaka kucheza kandanda.

"Jambo zuri zaidi ni kwamba yeye ni mchezaji huru (hana mkataba wowote kwa sasa)! Na anaweza kucheza nafasi kadha," alitania meneja wa Sundowns Pitso Mosiname.

Kiungo wa kati Mercy Tau alisema alifurahia sana kufanya amzoezi na Bolt.

"Bolt, asante sana kwa kufika hapa leo, imekuwa heshima kubwa kucheza nawe, niliona kwamba ulifanikiwa hata kufunga bao!"

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Usain Bolt akifurahia wakati wa mazoezi na wachezaji wa Mamelodi Sundowns

Bolt amekiri kwamba ni jambo ngumu kubadilisha kutoka kuwa mwanariadha na kuwa mwanakandanda.

Hata hivyo, aliishukuru klabu hiyo kwa kumpa fursa ya kufanya mazoezi an kikosi.

"Ilikuwa mechi nzuri, siku ya furaha na nilifurahia sana. Nilimwambia kocha kwamba nikirejea Jamaica nitahitaji mazoezi zaidi kwa sababu siko sawa."

"Niliwaambia marafiki zangu twafaa kupanga safari kwenda Afrika Kusini ni nchi ya kupendeza, naipenda midundo hapa, ni sawa na Jamaica kiasi!"

Bolt alitia saini mkataba na kampuni ya mavazi ya Ujerumani ya Puma ambao pia ni wadhamini wa Sundownd akiwa bado mdogo mwaka 2003.

Amekuwa akiashiria hamu yake ya kuwa mwanakandanda baada yake kustaafu riadha, na anaamini kwamba anaweza kuwa sawa kiasi cha kuchezea timu ya taifa ya Jamaica.

Bolt amealikwa kufanya mazoezi wiki moja na klabu ya Ujerumani ya Borussia Dortmund mwezi Machi na anapanga kukubali mwaliko huo.

Alikubali kwamba kunaweza kuwa na shaka kiasi lakini amesema tangu akiwa mdogo alikuwa na ndoto ya kucheza kandanda.