Arsenal walazwa na Swansea City EPL

Petr Cech Haki miliki ya picha Reuters

Swansea City waliondoka kwenye eneo la hatari ya kushushwa daraja Ligi ya Premia kwa mara ya kwanza tangu Novemba baada ya kuwalaza Arsenal.

Kosa la ajabu kutoka kwa Petr Cech lilimpa nafasi Jordan Ayew kufunga bao na kuwaweka wenyeji kifua mbele kipindi cha pili kabla ya Sam Clucas kufunga bao lake la pili usiku wa Jumanne na kukamilisha ushindi wao wa 3-1.

Mesut Ozil alikuwa ametoa pasi safi na kumuwezesha Nacho Monreal kufunga bao la kwanza mechi hiyo dakika ya 33 kabla ya Clucas kuwasawazishia Swansea uwanjani Liberty Stadium dakika moja baadaye.

Swansea wameandikisha ushindi mtawalia mara ya kwanza msimu huu.

Vijana wa Arsene Wenger nao wameshinda mechi moja pekee kati ya 13 walizocheza ugenini msimu huu Ligi Kuu ya England.

"Najihisi kwamba kwa kujilinda leo tulikuwa dhaifu sana na tulifanya makosa makubwa. Vyema zaidi ni kutozungumzia bao la pili na la tatu," alisema Wenger baada ya mechi.

"Swansea walikuwa makini sana, wenye nidhamu na hamu ya kutaka kushinda. Nasikitika, na naamini kwamba hatukucheza kwa kiwango cha kutosha, naamini hatukuwa na nidhamu ya kutosha.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Sam Clucas alisawazishia Swansea dakika moja baada ya Nacho Monreal kufungua ukurasa wa mabao
Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Swansea wameshinda mechi tatu kati ya tano EPL chini ya Carvalhal

Swansea wameonekana kuimarika sana chini ya meneja mpya Carlos Carvalhal ambapo wameshindwa mechi moja pekee kati ya nane walizocheza.

Ushindi wao dhidi ya Arsenal ndio wao wa pili mtawalia dhidi ya klabu iliyo nafasi sita za juu kwenye jedwali.

Liverpool ambao wamekuwa wakifunga mabao sana msimu huu walizimwa Liberty Stadium pia.

Giroud amesema kwaheri?

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Olivier Giroud amehusishwa na kuhama Arsenal

Huku Gunners wakitatizika Liberty Stadium, kulikuwa na wasiwasi na utata zaidi kuhusu shughuli za Wenger soko la kuhama wachezaji mwezi huu.

Arsenal wanatumai watafanikiwa kumnunua Pierre-Emerick Aubameyang kabla ya soko kufungwa leo jioni, lakini hiyo itategemea Mfaransa Olivier Giroud kuhama kutoka Emirates kwenda Stamford Bridge.

Giroud alijumuishwa kikosi cha Arsenal, lakini alikaa benchi pamoja na Henrikh Mkhitaryan.

Mashabiki waliimba jina lake kipindi chote cha mechi na bila shaka atakoswa sana na baadhi ya mashabiki wa Gunner iwapo ataondoka.

Mada zinazohusiana