Kiongozi aliyehusika na kuapishwa kwa Raila akamatwa, vyombo vya habari vyafungwa

Raila Odinga akila kiapo cha kuwa rais wa wananchi wa Kenya Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Raila Odinga akila kiapo cha kuwa rais wa wananchi wa Kenya

Polisi nchini Kenya wamemkamata mbunge mmoja ambaye 'alihusika' pakubwa katika hafla ya kumuapisha kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga kuwa 'rais wa wananchi'.

Kukamatwa kwa mbunge huyo wa upinzani kunajiri wakati ambapo serikali imefunga vituo vitatu vya runinga mbali na vile vya redio.

Tom Kajwang alikamatwa na kundi la maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia nguo za raia, mjini Nairobi.

Kukamatwa kwa kiongozi huyo kunajiri muda mfupi baada ya onyo kutoka kwa waziri wa usalama kwamba watu waliohusika katika kumuapisha Raila Odinga watakamatwa na kushtakiwa.

Vituo kadhaa vya runinga nchini Kenya vimefungiwa baada ya mamlaka ya mawasiliano kuzima mitambo yao kwa kujaribu kupeperusha moja kwa mkutano huo wa upinzani

Sherehe ya kuapishwa kwa Raila ilichukuliwa na wengi kama mzaha lakini serikali imeshikilia kuwa ni kitendo cha uhaini na kuhakikisha taarifa hiyo haitawafikia Wakenya wengi waliokuwa wakiifuatilia tukio hilo.

Waziri wa usalama nchini Kenya Dr Fred Matiangi amesema kuwa runinga hizo zitaendelea kufungwa hadi uchunguzi kuhusu kuhusika kwao na kundi la pingamizi dhidi ya serikali NRM linalohusishwa na muungano wa Nasa alilolipiga marufuku utakapokamilika.

Image caption Tom Kajwang amekamatwa na maafisa wa polisi kwa kuongoza kiapo cha Raila Odinga

Vifaa vya kurusha matangazo vya vituo vya runinga vya Nation Media Group NTV, Citizen TV cha kampuni ya Royal Media services Limited na KTN vilizuiwa kurusha matangazo katika kituo cha kurusha matangazo cha Limuru huku kituo cha kitaifa cha KBC na K24 kinachohusishwa na Rais Uhuru Kenyatta vikiendelea na matangazo yao.

Tangazo hilo la Matiangi linajiri huku kukiwa na malalamishi miongoni mwa raia kufuatia hatua hiyo ya serikali.

Katibu mkuu wa shirika la wafanyikazi nchini Kenya COTU Francis Atwoli ameishutumu serikali kwa kuingilia uhuru wa vyombo vya habari.

Bwana Atwoli ambaye alizungumza mjini Nairobi amesema kuwa hatua hiyo ni kinyume na sheria na inaenda kinyume na katiba ya Kenya ambayo inatoa Uhuru wa vyombo vya habari na kupata habari.

''Serikali inafaa kuharakisha na kurejesha matangazo ya runinga hizo. Sio makosa tu bali pia ni kinyume cha katiba kuendelea na biashara yao ya kuwahabarisha Wakenya'', alisema Atwoli.

Kufungwa kwa vituo hivyo kunajiri baada ya mwenyekiti wa shirika la wahariri Kenya Linus Kaikai kudai kwamba rais Uhuru Kenyatta alikuwa ametishia kuvifunga vyombo vya habari vitakavyojaribu kupeperusha matangazo ya kuapishwa kwa viongozi wa NASA.

Kulingana na Kaikai , vitisho hivyo vilitolewa katika ikulu ya rais tarehe 26 Januari baada ya wamiliki wa vyombo vya habari kuitwa na kutakiwa kutorusha matangazo hayo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii