Tony Chapron: Refa aliyempiga teke mchezaji apigwa marufuku miezi sita

Referee Tony Chapron aiming a kick at Diego Carlos Haki miliki ya picha BT Sport
Image caption Mwamuzi Tony Chapron alimrushia teke mchezaji wa Nantes Diego Carlos

Mwamuzi ambaye alimrushia teke mchezaji na kisha akamfukuza uwanjani amepigwa marufuku kwa miezi sita.

Nusu ya adhabu hiyo hata hivyo - miezi mitatu - imeahirishwa.

Beki Diego Carlos alimgonga mwamuzi Tony Chapron kwenye kisigino katika kilichoonekana kama ajali tu dakika za mwisho za mechi na mwamuzi huyo akaanguka

Chapron alimrushia teke mchezaji huyo na kisha akampa kadi ya pili ya njano, kwa sababu ya kulalamika.

PSG walishinda mechi hiyo 1-0.

Mwamuzi huyo alisimamishwa kazi kwa muda usiojulikana baada ya mechi hiyo akisubiri kuadhibiwa.

Kamati ya nidhamu ya Ligi ya Ufaransa ilitoa adhabu dhidi yake Alhamisi.

Kadi hiyo dhidi ya Carlos ilibatilishwa kufuatia ombi kutoka kwa Chapron.

Chapron amekuwa mwamuzi katika ligi kuu ya Ufaransa tangu 2004 na amesimamia zaidi ya mechi 400 kipindi hicho, ikiwa ni pamoja na fainali ya Kombe la Ufaransa mwaka 2014.

Kabla ya kisa hicho, alikuwa ametangaza kwamba huu ungekuwa msimu wake wa mwisho kuhudumu kama mwamuzi.

Mada zinazohusiana