Kamati ya Olimpiki IOC ''haikupendezwa'' na uamuzi wa CAS dhidi ya Warusi.

Thomas Bach Haki miliki ya picha Getty Images

Uamuzi wa kubatilisha marufuku ya maisha kwa wanariadha 28 wa Urusi wanaotuhumiwa kutumia dawa za kusisimua misuli ulikuwa wa ' kuvunja moyo sana na wa kushtusha'', kulingana na mkuu wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach.

Siku ya Alhamisi, Mahakama ya kutatua kesi za michezo ilibatilisha kupigwa marufuku ya maisha kwa wanariahda hao 28 wa Urusi na kwa kiwango fulani ikaidhinisha marufuku ya wengine 11 waliokuwa wamekata rufaa.

''Hatungeweza kulikubali hili''alisema Mjerumani huyo mwenye umri wa iaka 64.

Alisema kuwa maafisa wa Olimpiki wameitaka CAS itoe ufafanuzi kuhusu uamuzi huo.

CAS iliamua kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuwa wanariadha hao walifaidika na mpango uliodhaminiwa na serikali wa kuwapa dawa za kusisimua misuli katika michezo ya olimpiki ya msimu wa baridi mwaka 2014 ambayo Russia ilikuwa mwenyeji.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Alexander Tretiakov wa Urusi alishinda dhahabu huko Sochi - kabla ya kupigwa marufuku ya maisha na IOC

Akizungumza katika kikao na vyombo vya dola mjini Pyeongchang, Korea Kusini, siku tano kabla ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki msimu wa baridi, Bach alisema kuwa IOC ilikuwa imeelezewa kuwa watasubiri hadi mwisho wa mwezi Februari kupokea uamuzi huo kwa kina.

Alisema kuwa IOC ilijua kile kilichotolewa na CAS kupitia taarifa iliyotolewa na ameongeza kuwa hilo haliridhishi kutokanana uzito wa kesi zenyewe.

''Tunahisi kuwa uamuzi huu unaonyesha haja ya kufanyiwa marekebisho ya dharura katika muundo wa ndani wa CAS,''alisema.

Bach alisema kuwa ICO itafikiria kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo baada ya kupata sababu kamili zilizoisababisha CAS kufikia uamuzi huo.

Siku ya Jumamosi, IOC ilisema kuwa wanariadha 13 kati ya 28 walioondolewa mashtaka wataangaliwa iwapi wataruhusiwa na jopo maalum la IOC kushiriki katika michezo ya Olimpiki ya Pyeongchang.

Lakini Bach alisema: ''Kutokuwepo kwa marufuku za CAS haimaanishi kuwa unastahili kualikwa na IOC kwasababu kupokea mualiko huo ni fahari kubwa kwa wanaraidha wasafi wa Urusi.''

Adam Pengilly, mwanachama wa IOC wa Uingereza ametaja uamuzi huo kama ''siku hatari na nyeusi kwa michezo, ambapo watu warongo na wezi wanarahusiwa kushinda''.

Mada zinazohusiana