Eritrea yang'ara mbele ya Rwanda kwa medali katika mashindano ya baiskeli

Debesay Mekseb wa Eritrea
Maelezo ya picha,

Debesay Mekseb wa Eritrea

Mchuano mkali umefanyika baina ya waendesha baiskeli wa Eritrea na Rwanda katika shindano la kuwania ubingwa wa Afrika katika mbio za baiskeli linaloendelea nchini Rwanda.

Mwendesha baiskeli wa Eritrea Debesay Mekseb ameibuka kidedea katika mbio za leo km 40 kila mwendesha baiskeli akikimbia peke yake na kuangalia aliyetumia muda bora.

Debesay alimshinda Mnyarwanda Bosco Nsengimana aliyemaliza wa pili.

Kwa ujumla Eritrea imekusanya medali nyingi zikiwemo pia za upande wa wanawake na upande wa chipukizi.

Maelezo ya picha,

Bosco Nsengimana alimaliza wa pili katika shindano la kilomita 40.

Miongoni mwa wengine walioshiriki ni waendesha baiskeli kutoka Uganda ambao hata hivyo waliambulia patupu na hawakumfurahisha Kocha wao Hamza Adam.

Pia waendesha baiskeli kutoka Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo hawakuachwa nyuma. Mwindo Jimmy anasema wanajitahidi kadri ya uwezo wao licha ya barabara za milima kuwatatiza.

Wakati huo huo shirikisho la mchezo wa mbio za baiskeli umemtangaza mwendesha baiskeli wa Rwanda, Areruya Joseph kuwa ndiye kinara Afrika nzima katika kuendesha baiskeli kufuatia hasa yeye kushinda mashindano mengi makubwa ya hivi karibuni.

Areruya leo ameshinda dhahabu katika upande wa waendesha baiskeli walio chini ya umri wa miaka 23.