Chelsea watoka sare ya 1-1 na Barcelona UEFA

Willian Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bao la Willian kipindi cha pili lilikuwa lake la 11 kufungia Chelsea mashindano yote msimu huu

Klabu za Chelsea na Barcelona zimemetoka sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza wa raundi ya 16 katika michuano Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya UEFA.

Katika mchezo huo Chelsea ndio walikuwa wa kwanza kufunga bao la dakika 62 kipindi cha pili likifungwa na Willian Borges Da Silva kufutia pasi ya Eden Hazard.

Kabla ya kufunga, Willian alikuwa amegonga mwamba wa goli mara mbili kipindi cha kwanza jambo lililowatia matumaini Blues.

Muda mfupi baadaye Barcelona wakafanikiwa kusawazisha bao hilo mnamo dakika ya 75 kipindi cha pili lililofungwa na Lionnel Messi kufuatia pasi ya Andrea Iniesta.

Matokeo hayo uwanjani Stamford Bridge yana maana kwamba hakuna klabu hata moja ya England kufikia sasa imeshindwa mechi yake ya kwanza hatua ya 16 bora.

Liverpool walilaza Porto 5-0, Manchester City wakacharaza Basel 4-0, Tottenham wakatoka sare 2-2 nyumbani kwa Juventus nao Manchester United watacheza ugenini dhidi ya Sevilla Jumatano, 21 Februari.

Chelsea na Barca watarudiana tena mwezi Machi katika dimba la Nou Camp mnamo 14 Machi.

Messi amaliza ukame dhidi ya Chelsea

Messi alikuwa amecheza dakika 730 dhidi ya Chelsea bila kufanikiwa kutikisa wavu lakini Jumanne bahati yake ilisimama na akawapa Barca bao muhimu la ugenini.

Mchezaji huyo wa Argentina mwenye miaka 30 alikuwa amecheza mechi nane Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Chelsea bila kufunga - na kwa sehemu kubwa ya mechi, alionekana kana kwamba angeondoka mikono mitupu.

Walinzi wa Chelsea walifanikiwa kumkaba kwa kipindi kirefu.

Lakini beki Andreas Christensen alifanya kosa akitoa pasi na Andres Iniesta akaupata mpira na kumsambazia Messi ambaye hakufanya masihara na akambwaga kipa Courtois, hatua iliyomjaza tabasamu mkufunzi wa Barca Ernesto Valverde.

Haki miliki ya picha Reuters
Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Chelsea yatoa sare ya 1-1

Katika mchezo mwingine Bayern Munich waliwakaribisha Besktas, mchezo huo umemalizika kwa Bayern Munich kuibuka na ushindi wa mabao 5-0, mabao ya Bayern yamefungwa na Thomas Muller, Kingsley Coman na Robert Lewandowski. Michuano hiyo ya klabu bingwa Ulaya inaendelea tena leo Jumatano kwa michezo miwili, Sevilla wanawaalika Manchester United na Shakha Donestk ni wenyeji wa As Roma.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Willian aligonga mwamba wa goli mara mbili kipindi cha kwanza

Nini kitafuata?

Chelsea watacheza mechi tatu kabla ya kukutana na Barcelona kwa mechi ya marudiano, mechi hizo zikijumuisha mechi za ugenini Ligi ya Premia dhidi ya klabu mbili za Manchester.

Watakutana na Manchester United Jumapili, 25 Februari (14:05 GMT) na kisha wakutane na Manchester City Jumapili itakayofuata (16:00 GMT).

Barcelona watarejea uwanjani La Liga Jumamosi, 24 Februari kwa mechi ya nyumbani dhidi ya klabu ya Girona ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya nane.

Mada zinazohusiana