De Gea awasaidia Manchester United kutoka sare na Sevilla Ligi ya Mabingwa Ulaya UEFA

David de Gea

Chanzo cha picha, Rex Features

Mlindalango wa Manchester United David de Gea alifanya kazi ya ziada kuzuia makombora ya wapinzani wao Sevilla Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mechi ya hatua ya 16 bora na kuwasaidia kutoka sare Jumatano.

Kipa huyo Mhispania aliwazuia Joaquin Correa na Steven N'Zonzi kufunga kwa ustadi mkubwa, na kisha akatumia mkono mmoja muda mfupi kabla ya mapumziko kuzuia mpira wa kichwa wa Luis Muriel.

United, waliokuwa wanacheza mechi yao ya kwanza ya muondoano Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika kipindi cha miaka minne hawakushambulia sana.

Romelu Lukaku alipoteza nafasi nzuri zaidi kwao mpira wake ulipopaa juu ya lango mapema, kabla ya nguvu mpya Marcus Rashford kutupa mpira nje dakika za mwisho mwisho.

Paul Pogba alianza mechi kwenye benchi, lakini akaingizwa uwanjani dakika 17 kabla ya mechi kumalizika baada ya Ander Herrera kuumia.

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha,

David de Gea amecheza mechi 19 bila kufungwa msimu huu

Sevilla walimaliza mechi wakiwa wameshambulia goli mara 25 lakini mseto wa ustadi wa De Gea na makosa ya washambuliaji wao viliwazuia kuondoka na ushindi uwanja wao wa nyumbani.

Manchester United ndio watakaokuwa na furaha klabu hizo zinapojiandaa kukutana tena kwa mechi ya marudiano Old Trafford Jumanne, 13 Machi.

Vijana hao wa Jose Mourinho wameshinda mechi 15 kati ya 18 walizocheza nyumbani msimu huu.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Paul Pogba hajacheza dakika 90 tangu alipocheza mechi ambayo United walishinda 1-0 ugenini Burnley 20 Januari

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

De Gea alizuia makombora manane - idadi ya juu zaidi kwa kipa wa Manchester United mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya tangu Edwin van der Sar aliyezuia makombora sawa dhidi ya Barcelona Mei 2011

Tano kati ya mechi saba za karibuni zaidi ambazo Manchester United wamecheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya nchini Uhispania zimemalizika kwa sare tasa.

Mechi hiyo ya Jumatano ilikuwa yao ya tisa kati ya 11 za karibuni zaidi mashindano yote kwa United kutofungwa, na yao ya 23 mashindano yote msimu huu.

Nini kinafuata?

Manchester United wana mechi kubwa Ligi ya Premia watakapokuwa wenyeji wa Chelsea mnamo Jumapili 25 Februari (14:05 GMT).