Soccer Aid: Usain Bolt kucheza soka uwanja wa Manchester United Old Trafford

Usain Bolt with a football

Chanzo cha picha, Unicef/Cooper

Bingwa wa Olimpiki Usain Bolt hatimaye atapata fursa ya kuchezea soka katika uwanja wa Manchester United wa Old Trafford.

Mshindi huyo wa dhahabu mara nane katika Olimpiki atakuwa nahodha wa timu ya pamoja na watu mashuhuri na wanasoka ambayo itashiriki mechi ya Soccer Aid ambayo itaandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto (Unicef) mnamo 10 Juni.

"Ni ndoto yangu kufanikiwa kama mchezaji wa soka ya kulipwa. Kucheza dhidi ya baadhi ya wachezaji nyota, hilo litakuwa jambo la kufurahisha sana," raia huyo wa Jamaica amesema.

Manchester United wameandika kwenye Facebook: "Inafanyika hatimaye ... Usain Bolt ataonyesha ustadi wake katika kusakata kambumbu katika Old Trafford majira yajayo ya joto #SoccerAid!

Robbie Williams atakuwa nahodha wa timu pinzani kutoka England wakati wa mechi hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Niall Horan na Louis Tomlinson walicheza mechi ya Soccer Aid mwaka 2016

Usain awali amezungumzia nia yake ya kutaka kucheza soka ya kulipwa baada yake kustaafu riadha mwaka jana.

Wikendi, aliandika ujumbe wa utani kwenye Twitter - ambao ulizua uvumi sana - akidokeza kwamba alikuwa amejiunga na klabu fulani.

"Robbie na timu yake ya England wawe macho, kwani haitakuwa rahisi kwao," amesema Usain, na kuongeza kwamba amepanga "kitu maalum cha kusherehekea" timu yake ikishinda.

Bolt, 31, ni shabiki wa Manchester United, na wakati mmoja alipiga simu kwenye runinga ya klabu hiyo, MUTV, bila kutarajiwa.

"Nimekuwa nikisemamuda mrefu kwamba ninataka sana kufanikiwa katika mchezo wa timu kwa sababu uwanjani ni bidii ya mtu binafsi," alisema wakati huo.

"Huwa najiimarisha upesi na kufahamu ninafaa kufanya nini punde ninapopata kazi. Ninapopata maagizo, huyafuatilia vyema sana," alisema.

Chanzo cha picha, Reuters

Mechi hiyo ya Soccer Aid itawaleta pamoja watu mashuhuri na wachezaji nyota wa zamani wa soka.

Mechi hiyo, ambayo huchezwa kila miaka miwili kufikia sasa imechangia kuchangisha jumla ya £24 milioni tangu kuzinduliwa kwake 2006.

Mechi hiyo awali imewashirikisha wachezaji wa zamani kama vile Maradona, Alan Shearer na Ronaldinho wakicheza dhidi ya watu mashuhuri kama vile Mark Wright, Jack Whitehall na Olly Murs.

Will Ferrell, Gordon Ramsay, Mike Myers na Craig David pia wamewahi kucheza.

"Kutwaa tena taji hili kwa niaba ya England litakuwa jambo zuri sana Usain akiongoza Soccer Aid World XI (Timu ya Dunia)," alisema Robbie Williams, ambaye ni mwanzilishi mwenza wa Soccer Aid.

"Nasubiri sana kuongoza timu ya England."

Tiketi za mechi hizo zinauzwa £10 na £50.